" DIWANI WA KATA YA SOLWA MHE. DOTTO SAMSON (IPILILO) AWAHIMIZA WANANCHI KUDUMISHA AMANI, AAHIDI KUENDELEA KUSUKUMA MAENDELEO

DIWANI WA KATA YA SOLWA MHE. DOTTO SAMSON (IPILILO) AWAHIMIZA WANANCHI KUDUMISHA AMANI, AAHIDI KUENDELEA KUSUKUMA MAENDELEO

Na Mapuli Kitina Misalaba

Diwani wa Kata ya Solwa, Mhe. Dotto Samson maarufu kwa jina la Ipililo, leo Juni 15, 2026 amefanya mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Solwa chenye vitongoji vitano, ambapo amewahimiza wananchi kuendelea kudumisha amani, umoja na utulivu huku akiahidi kuendelea kupigania maendeleo ya kijiji hicho na Kata ya Solwa kwa ujumla.

Akizungumza katika mkutano huo uliofanyika kijijini hapo, Mhe. Ipililo amesema kuwa maendeleo hayawezi kupatikana bila kuwepo kwa amani na ushirikiano kati ya wananchi na viongozi, hivyo amewataka wakazi wa Solwa kuendelea kuwa walinzi wa amani na mshikamano uliopo katika eneo lao.

Amesema mkutano huo ni sehemu ya mwendelezo wa ziara zake za kutembelea vijiji mbalimbali vya Kata ya Solwa kwa lengo la kuwashukuru wananchi kwa imani kubwa waliyoionesha kwake wakati wa uchaguzi mdogo uliofanyika kufuatia kifo cha aliyekuwa Diwani wa kata hiyo.

Katika mkutano huo, Diwani huyo pia amelipongeza Jeshi la Jadi Sungusungu kwa mchango wake katika kuimarisha ulinzi na usalama wa wananchi, huku akiwataka kuendelea kushirikiana na Serikali pamoja na vyombo vya dola katika kulinda amani ya maeneo yao.

Aidha, amewasisitiza viongozi wa jeshi hilo wanaofahamika kama Watemi kuwa waadilifu, wa mfano mzuri kwa jamii na kuendelea kuyaongoza majesho yao kwa kuzingatia sheria, maadili na maslahi ya wananchi.

Mkutano huo wa hadhara pia uliwapa wananchi fursa ya kueleza kero, changamoto na malalamiko mbalimbali yanayowakabili katika maisha yao ya kila siku. Baadhi ya wananchi waliwasilisha maombi ya kuboreshwa kwa huduma za usafi wa mazingira, ikiwemo kutengenezwa kwa dampo maalum la kutupia taka ili kuimarisha afya na usafi wa mazingira katika kijiji hicho.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Solwa, Bwana John Bernard Kaselya, akizungumza kwa niaba ya wananchi, ameeleza kuwa pamoja na jitihada zinazofanywa na Serikali, bado kijiji hicho kinakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazohitaji ufumbuzi wa haraka.

Ametaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni ubovu wa miundombinu ya barabara katika maeneo mbalimbali ya kijiji, bei ya maji, upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama pamoja na changamoto ya umeme katika baadhi ya vitongoji ambavyo bado havijafikiwa kikamilifu na huduma hiyo.

Akijibu hoja na maswali yaliyoulizwa na wananchi, Mhe. Ipililo amesema ataendelea kuzifikisha changamoto zote katika mamlaka zinazohusika ili ziweze kupatiwa ufumbuzi kwa wakati.

Amesema tayari Serikali imepeleka na kupokea kiasi cha takribani shilingi milioni 10 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya stendi ya Solwa, ikiwemo ukarabati wa vyoo pamoja na kuziba mashimo na mabonde yaliyokuwa yakisababisha usumbufu kwa watumiaji wa eneo hilo.

Vilevile, amesema kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Shinyanga, tayari mchakato wa kuboresha barabara inayotoka Solwa Senta kupitia Zahanati ya Ipililo umeidhinishwa, jambo ambalo litasaidia kupunguza changamoto ya usafiri na usafirishaji iliyokuwa ikiwakabili wananchi kwa muda mrefu.

Diwani huyo ameongeza kuwa ataandaa kamati maalum itakayoshirikiana na viongozi wa vijiji na wananchi kufuatilia changamoto nyingine zilizobainishwa ili kuhakikisha zinapatiwa ufumbuzi kwa haraka.

Ziara hiyo ya Mhe. Ipililo imeambatana na wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Solwa. Mkutano huo pia umehudhuriwa na viongozi mbalimbali pamoja na wataalamu kutoka ofisi ya kata, akiwemo Afisa Mifugo, Afisa Maendeleo ya Jamii, Mganga Mfawidhi na Afisa Afya wa kata, ambao wamepata nafasi ya kujibu maswali na kutoa ufafanuzi kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa katika sekta zao.

Ushiriki wa wananchi kwa wingi pamoja na uwepo wa watu wenye mitazamo tofauti ya kisiasa katika mkutano huo umeelezwa kuwa ni ishara ya kuendelea kuimarika kwa mshikamano, uvumilivu wa kisiasa na ushirikiano katika Kijiji cha Solwa, hali ambayo ni muhimu katika kuharakisha maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Solwa, John Bernard Kaselya, akieleza changamoto zinazowakabili wananchi wa kijiji hicho mbele ya Diwani wa Kata ya Solwa na viongozi mbalimbali waliohudhuria mkutano wa hadhara.

 SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment

Previous Post Next Post