
Na Mapuli Kitina Misalaba
Viongozi wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania
(JMAT) Mkoa wa Shinyanga wameonya vikali vitendo vya hujuma dhidi ya
miundombinu ya ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Shinyanga, wakisisitiza kuwa
kulinda miradi ya maendeleo ni sehemu ya kudumisha amani na ustawi wa jamii.
Onyo hilo limetolewa kufuatia ziara ya viongozi hao
katika mradi huo ambapo walijionea hatua ya utekelezaji wake, huku ujenzi ukiwa
umefikia asilimia 97.3 ya ukamilishaji.
Akizungumza mara baada ya ziara hiyo, Mwenyekiti wa
JMAT Mkoa wa Shinyanga, Sheikh Balilusa Khamisi, amesema kuwa wataendelea
kutumia majukwaa ya kidini kuhubiri amani, uzalendo na kuwahimiza wananchi
kulinda mali za umma ili kukomesha vitendo vya wizi na uharibifu wa
miundombinu.
Amesema vitendo vya hujuma vinahatarisha juhudi za
serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo, akibainisha kuwa serikali
imewekeza fedha nyingi katika miradi hiyo kwa manufaa ya wote. Ameongeza kuwa
kukamilika kwa uwanja huo kutafungua fursa nyingi za kiuchumi na kibiashara kwa
wakazi wa mkoa wa Shinyanga.
Viongozi hao wa JMAT wamesema utekelezaji wa mradi huo
unaonyesha dhamira ya dhati ya serikali katika kupanga, kuwekeza na kusimamia
miradi ya maendeleo kwa ufanisi, hivyo ni wajibu wa wananchi kushirikiana
kuulinda.
Kwa upande wake, msimamizi wa uwanja huo, Lugano
Mwinuka, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya
Ndege Tanzania (TAA), Abdul Athuman Mombokaleo, amesema mradi huo unatarajiwa
kukamilika hivi karibuni na utaimarisha huduma za usafiri wa anga ndani na nje
ya mkoa huo.
Amesema kukamilika kwa uwanja huo kutaongeza fursa za
biashara, kuchochea shughuli za kiuchumi na kuongeza mapato ya serikali kupitia
kodi na tozo mbalimbali.
Hata hivyo, Mwinuka amebainisha kuwepo kwa changamoto
ya wizi wa miundombinu, akieleza kuwa Januari mosi mwaka huu watu wasiojulikana
waliiba baadhi ya vyuma vya uzio wa uwanja huo, hali inayohitaji ushirikiano wa
wananchi na vyombo vya ulinzi na usalama kukomesha vitendo hivyo.
Naye Mhandisi Chiyando Matoke, akizungumza kwa niaba
ya Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), amesema mradi huo
unatekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 44.8, ambapo hadi sasa serikali
imelipa shilingi bilioni 38.6 kwa mkandarasi.
Ametumia nafasi hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuwekeza katika
miradi ya miundombinu inayochochea ukuaji wa uchumi na kuboresha huduma za
kijamii nchini, ikiwemo mkoa wa Shinyanga.
Aidha, ameeleza kuwa serikali tayari imelipa fidia kwa
wananchi wote waliopisha utekelezaji wa mradi huo.
Mradi wa ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Shinyanga
unafadhiliwa na Serikali ya Tanzania na unatekelezwa na mkandarasi wa China,
Hennan International Corporation Group Co. Ltd (CHICO), huku ukitarajiwa kuwa
chachu ya maendeleo na ustawi wa kiuchumi katika mkoa huo.
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254






Post a Comment