" WATUMISHI WA UMMA KUPATIWA MAFUNZO YA USALAMA NA MATUMIZI YA TEHAMA

WATUMISHI WA UMMA KUPATIWA MAFUNZO YA USALAMA NA MATUMIZI YA TEHAMA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, akiwasilisha Hotuba ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 leo Aprili 17,2026 bungeni Dodoma.

Na.Alex Sonna,Mzalendo blog-DODOMA

Serikali kupitia Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) imeweka mkazo katika kuimarisha usalama, ufanisi na ushirikiano wa mifumo ya TEHAMA katika taasisi za umma kwa mwaka wa fedha 2026/27, ikiwa ni sehemu ya mageuzi ya kidijitali yanayolenga kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Hayo yamesemwa leo Aprili 17,2026 bungeni Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, akiwasilisha Hotuba ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027.

Amesema kuwa  e-GA itasimamia na kutathmini hali ya usalama wa mifumo na miundombinu ya TEHAMA katika taasisi 571 nchini, kwa lengo la kubaini maeneo yenye udhaifu na kutoa mapendekezo ya maboresho pamoja na kufuatilia utekelezaji wake ili kuhakikisha mifumo inafanya kazi kwa ufanisi na usalama wakati wote.

Aidha, mamlaka hiyo itaendelea kuimarisha mifumo jumuishi ya TEHAMA pamoja na mifumo ya kisekta na kitaasisi ili kuhakikisha huduma za serikali zinatolewa kwa urahisi, usalama na kwa gharama nafuu zaidi.

"Katika kupunguza urudufu wa mifumo, e-GA imepanga kufanya uchambuzi, usanifu na ujenzi wa mifumo mipya ya kisekta kwa taasisi zenye majukumu yanayofanana, hatua itakayosaidia kuimarisha ufanisi na kupunguza wingi wa mifumo isiyo na tija serikalini."amesema Mhe.Ridhiwani

Vilevile, mamlaka hiyo itaunganisha mifumo ya taasisi mbalimbali kupitia Mfumo wa Government Enterprise Service Bus (GovESB), ili kuwezesha taasisi za Serikali kubadilishana taarifa kwa urahisi na kwa wakati.

Katika kuendana na maendeleo ya teknolojia, e-GA itafanya utafiti na ubunifu wa matumizi ya teknolojia mpya za TEHAMA ili kuibua huduma mpya kwa wananchi na kuhakikisha matumizi salama ya teknolojia zinazoibuka.

Aidha, mtandao wa Serikali (Government Network) utaimarishwa na kupanuliwa ili kufikia wilaya zote nchini, hatua itakayowezesha taasisi nyingi kutumia mifumo ya serikali mtandao kama vile e-Office kwa ufanisi zaidi.

Mamlaka pia itaendelea kusimamia na kuendesha miundombinu shirikishi ya TEHAMA ikiwemo vituo vya kuhifadhi taarifa, mifumo ya serikali na vituo vya kujikinga na majanga ili kuhakikisha uendelevu wa huduma za kidijitali.

Kwa upande wa rasilimaliwatu, e-GA itatoa mafunzo kwa watumishi wa umma kuhusu usimamizi wa mifumo ya TEHAMA pamoja na matumizi salama ya teknolojia, ili kuongeza ufanisi na kupunguza makosa ya kiutendaji.

Kwa ujumla, mpango huu unaonesha dhamira ya Serikali kupitia e-GA ya kuimarisha matumizi ya TEHAMA, kuongeza usalama wa mifumo ya kidijitali na kuboresha utoaji wa huduma za umma kwa njia ya kisasa na yenye tija zaidi.

SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA

 
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment

Previous Post Next Post