
Na Mapuli Kitina Misalaba
Jumla ya watuhumiwa 63 wamekamatwa kwa makosa
mbalimbali mkoani Shinyanga kufuatia operesheni zilizofanywa na Jeshi la Polisi
katika kipindi cha mwezi Aprili 2026.
Kwa mujibu wa Kamanda wa jeshi la Polisi Mkoa wa
Shinyanga kamishna msaidizi mwandamizi wa Polisi Janeth Magomi, operesheni hizo
zililenga kukabiliana na uhalifu na kudhibiti vitendo vinavyokiuka sheria
ambapo zimefanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao pamoja na kukamatwa kwa
vielelezo mbalimbali.
Vielelezo vilivyokamatwa ni pamoja na mafuta ya dizeli
lita 295, bangi gramu 1,100, mirungi kilogramu 103, noti bandia zenye thamani
ya shilingi 81,000, simu 98, betri za simu 86, pomba na moshi lita 55, pikipiki
14, vipande vya chuma 21, redio 8, viti vya plastiki 6, mifuko 13 ya mawe
yanayodhaniwa kuwa madini, spika 5, mashine ya kukatia mikate 1 na mbuzi 7
waliokamatwa katika wilaya za Kahama na Ushetu.
Aidha, polisi wamesema kesi saba zimefikishwa
mahakamani ambapo watuhumiwa saba wamehukumiwa kifungo cha miezi sita hadi
miaka minne jela katika kesi za wizi. Kesi nyingine zinahusisha kutishia kwa
maneno, kushambulia na kudhuru mwili, pamoja na kuharibu mali, ambapo wahusika
wamehukumiwa vifungo mbalimbali jela.
Katika hatua nyingine, Kikosi cha Usalama Barabarani
kimeendelea na operesheni dhidi ya madereva wanaokiuka sheria za usalama
barabarani, ambapo jumla ya makosa 4,260 yalibainika. Miongoni mwa makosa hayo
ni ya magari 3,030 pamoja na makosa ya bajaji na pikipiki 1,230, huku wahusika
wakitozwa faini katika maeneo husika.
Polisi pia wamemfungia leseni dereva mmoja kwa muda wa
miezi mitatu baada ya kukutwa akiendesha gari kwa mwendokasi wa zaidi ya
kilomita 80 kwa saa.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga limewataka wananchi
kuendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kutoa taarifa
zitakazosaidia kukomesha uhalifu na kuimarisha amani katika jamii.
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment