
MWANAMKE mmoja mkazi wa Jimbo la Harari nchini Ethiopia amejifungua watoto watano kwa mara moja baada ya kuhangaika kutafuta mtoto kwa miaka 12, jambo lililoonekana kuwa adimu zaidi nchini humo.
Mwanamke huyo aliyejitambulisha kwa jina la Bedriya Adem, amesema yeye na mumewe walijawa na furaha kubwa kwa “kubarikiwa kupata watoto watano kwa wakati mmoja.”
Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 35 alijifungua wavulana wanne na msichana mmoja, ambao wote wako katika “afya njema kabisa,” katika Hospitali Maalum ya Hiwot Fana, kwa mujibu wa hospitali hiyo.
“Siwezi kuelezea furaha yangu kwa maneno,” alisema, huku akieleza jinsi alivyokuwa amejaa huzuni na maumivu hadi pale maombi yake yalipojibiwa.
Mkurugenzi wa matibabu wa hospitali hiyo, Dk. Mohammed Nur Abdulahi, alisema mama na watoto bado wako chini ya uangalizi wa kitabibu hospitalini. Na kwamba watoto hao walikuwa na uzito kati ya kilo 1.3 na 1.4.
Alisema watoto wanaozaliwa wakiwa na uzito zaidi ya kilo moja huwa na nafasi kubwa ya kuishi na kukua kwa afya njema.
Daktari huyo pia alieleza kuwa Bedriya alipata ujauzito huo kwa njia ya kawaida, bila msaada wa teknolojia ya upandikizaji wa mayai nje ya mwili (IVF), huduma ambayo hospitali hiyo haitoi.
IVF inaweza kuongeza uwezekano wa kupata watoto wengi kwa wakati mmoja iwapo zaidi ya kiinitete kimoja kitapandikizwa.
Uwezekano wa kupata watoto watano kwa njia ya kawaida ni takribani mmoja kati ya watu milioni 55.
Daktari alisema kujifungua kulifanyika kwa njia ya upasuaji siku chache zilizopita.
“Alipata huduma za matibabu mara kwa mara wakati wa ujauzito wake na alijulishwa kuwa alikuwa na ujauzito wa zaidi ya mtoto mmoja. Alipata msaada kamili wa kitabibu muda wote,” alisema Mohammed, akielezea pia furaha yake.
Mama aliyejifungua watoto watano kwa mara moja.
Bedriya alisema hapo awali aliambiwa ana ujauzito wa watoto wanne, lakini alipojifungua akawa na mmoja zaidi.
“Niliomba mtoto mmoja tu, lakini Allah akanipa watano,” alisema, akizungumzia alivyohisi wakati wa kusubiri kwake kwa muda mrefu.
Mama huyo alisema mumewe tayari alikuwa na mtoto kutoka ndoa nyingine ambaye waliishi naye.
“Alikuwa akiniambia kuwa na mtoto huyo kulitosha na nisiwe na wasiwasi, lakini moyoni nilikuwa naumia kisaikolojia na kihisia kwa sababu kijiji kizima kilikuwa kikihoji kwanini sipati mtoto,” alisema.
“Niliyoyapitia zamani sasa yanaonekana kama ndoto ya mbali ambayo sitaki hata kuikumbuka. Nilitumia miaka 12 katika maumivu, nikijificha na kuomba kila mara nipate watoto hatimaye Allah alinijibu,” alisema.
Alisema yeye ni mkulima mdogo na hana uhakika jinsi atakavyoweza kuhudumia familia yake iliyoongezeka ghafla. “Lakini naamini Allah atasaidia kupitia jamii yangu na serikali.”
Watoto hao watano wamepewa majina ya Naif, Ammar, Munzir, Nazira na Ansar.
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment