Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa kliniki ya kusikiliza na kushughulikia malalamiko ya wananchi dhidi ya Mgodi wa Barrick North Mara.
Meneja wa Idara ya Mahusiano ya Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara, Francis Uhadi, akizungumza wakati wa uzinduzi wa kliniki hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele na viongozi wa Barrick wakiwa katika picha ya pamoja na wadau wengine baada ya uzinduzi wa awamu ya pili ya Kiliniki ya Kusikiliza na Kushughulikia Malalamiko ya Wananchi.
****
Mgodi wa Barrick North Mara umezindua kliniki ya awamu ya pili maalum ya kusikiliza malalamiko , kero na migogoro ya wananchi ili kupata utatuzi wa kudumu kwenye vijiji 11 vinavyozunguka mgodi huo kwa ajili ya kuendelea kuboresha mahusiano kati ya mgodi na jamii.
Kliniki hiyo ya malalamiko inatoa fursa ya kuwakutanisha wananchi wanaozunguka mgodi huo na kutoa nafasi ya majadiliano ya kina, uwazi, kuboresha mahusiano ya kuaminiana na uwajibikaji kati ya jamii, mgodi na serikali na kuhakikisha malalamiko yanachukuliwa, yanapitiwa , kuweka kwenye kumbukumbu na hatimaye kushughulikiwa.
Kliniki hiyo inayojumuisha wajumbe kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Mgodi wa Barrick North Mara, Tume ya Haki za binadamu na utawala wa bora , asasi za kiraia- mashirika yasiyo ya kiserikali pamoja na wadau wengine, inalenga kuimarisha mahusiano kati ya mgodi na wananchi wa vijiji vinavyozunguka eneo hilo ili kuwezesha uwekezaji endelevu wenye maslahi mapana kwa wilaya , Mkoa na taifa kwa ujumla.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa kliniki hiyo ya pili katika kijiji cha Mjini Kati kilichopo Nyamongo, Wilayani Tarime, Mkuu wa Wilaya hiyo, Meja Edward Gowele alisema hatua hiyo itasaidia kupunguza na hatimaye kumaliza malalamiko na migogoro kati ya mgodi na jamii inayozunguka mgodi huo.
“Niupongeze mgodi wa Barrick North Mara kwa kufanya kliniki kwa awamu ya pili ni hatua kubwa na ni matumiani yangu kuwa itapunguza malalamiko na migogoro. Ili kujenga jamii ya amani na utulivu lazima tusikilizane na kutatua migogoro iliyopo,” alisema.
Meja Gowele alitumia nafasi hiyo pia kutoa wito kwa wanavijiji kujitokeza kuwasilisha malalamiko yao kwenye kliniki hiyo ili yapatiwe utatuzi kwa maendeleo na ustawi wa pande zote mbili.
Aidha, aliitaka kamati ya kliniki hiyo na viongozi wa vijiji kuhakikisha wananchi wanapata taarifa kwa wakati kuhusu mikutano ya kusikiliza na kupokea malalamiko yao itakayofanyika katika kila kijiji.
“Nimezindua rasmi kliniki hii, ipite kila kijiji na kusikiliza kila mwananchi mwenye malalamiko bila ubaguzi wala upendeleo,” Meja Gowele alisisitiza.
Ili kuongeza uwazi, uwajibikaji na ushiriki mpana wa wadau wote, klinki hiyo ina kamati inayojumuisha wafanyakazi wa mgodi, madawati ya malalamiko kutoka ofisi za Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, asasi za kiraia na wawakilishi wa jamii.
Gowele alisisitiza kwamba kwa watu waliopo ndani ya eneo la leseni ya Barrick North Mara kutii sheria bila shuruti na kuondoka ili kutokwamisha shughuli za mgodi huo.
Pamoja na mambo mengine , Mkuu wa Wilaya hiyo aliwataka watendaji wa Halmashauri ya Tarime kutoa ushirikiano kwenye miradi ya kimkakati katika wilaya hiyo ikiwemo ujenzi wa soko la dhahabu la Nyamongo na ujenzi wa stendi ya kisasa ya Nyamwaga.
“Nimeelezwa kwamba ili miradi hiyo iweze kuendelea ni lazima hati za maeneo husika zipatikane kwa wakati, watendaji hakikisheni unakamilisha taratibu zote zinazohitajika bila kuchelewesha maendeleo” , aliongeza.
Alisisitiza kwamba kukamilika kwa miradi hiyo ni hatua muhimu yenye kutia matumaini na kuongeza mahusiano mazuri kati ya wananchi na mgodi.
Akizungumza kwenye uzinduzi rasmi wa kliniki hiyo Mkoa Mara , Wilaya ya Tarime, Tarafa ya Nyamongo , Meneja Uhusiano wa Jamii wa Mgodi wa Barrick North Mara, Franscis Uhadi alisema kwamba mahusiano kati ya mgodi na wananchi umezidi kuimarika ila bado kuna changamoto ambazo zinahitaji utatuzi wa kudumu ili kurahisisiha shughuli za uchimbaji na kuboresha mahitaji ya wananchi kupitia sheria na kanuni ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR).
Alisema kwamba moja ya changamoto inayoendelea kujitokeza ni malipo ya fidia kwa wananchi akisema kwamba baadhi ya wananchi kwenye jamii kuendelea kugoma malipo ya fidia kwa kudai kwamba hajaridhishwa.
“Wananchi 728 walifanyiwa tathimini katika eneo la Nyabirama na malipo yao yapo tayari , kati yao 667 wamepokea fidia na kupisha shughuli za mgodi huku 61 wakiendelea kusubiri ambapo watu 44 ni wa familia moja,” alisema Uhadi.
Uhadi alisema kwamba mgodi wa umeendelea kutekeleza miradi ya jamii kupitia kanuni na sheria za Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) ambapo miradi 103 imepagwa kutekelezwa mwaka huu na huku 70 ikiwa tayari imekamilika na mengine ikiwa kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji.
Alisema kwamba kliniki hiyo itazunguka kwenye vijiji vyote 11 vinavyozunguka mgodi huo ili kuwafikia wananchi moja kwa moja na kuweza kutatua changamoto zao moja kwa moja.
Kwa upande wake, Mwenyekiti mpya wa Kamati ya Maendeleo ya Jamii (CDC) katika mgodi wa Barrick North Mara, Bogomba Rashid, alisema hatua hiyo ya kusikiliza na kutatua migogoro itasaidia pia kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika vijiji vinavyozunguka mgodi huo.
“Tukimaliza migogoro ambayo haina sababu ya kuwepo tutaendelea kufanya shughuli za maendeleo zaidi katika maeneo yetu,” alisema Bogomba ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Kemambo.
Baadhi ya wananchi waliohudhuria shughuli hiyo ya uzinduzi wa kliniki walipongeza hatua hiyo ya mgodi wa Barrick North Mara kwa sababu itapunguza migogoro na kupanua wigo wa ushirikiano na kukuza mahusiano kati ya mgodi na jamii.
Mkazi wa Kijiji cha Kewanja , Mwita Omahe alisema kwamba pamoja na kuimarika kwa mahusiano kati ya jamii na mgodi ila bado kuna changamoto ya barabara mbovu za mitaa ambazo zinahitaji kushughulikiwa.
Katika awamu ya kwanza ya kliniki hiyo iliweza kuwafikia wananchi zaidi ya 1,688 na kero zilizopokelewa zilikuwa 137.
Vijiji vinavyozuguka mgodi huo ambavyo vitanufaika na kliniki hiyo ya wiki moja ni Mjini kati, Nyangoto, Kewanja, Matongo, Nyabichune, Kerende, Nyakunguru, komarera, Genkuru, Msege na Nyamwaga.
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254










Post a Comment