" BENKI YA CRDB YAWEKA REKODI, YATENGENEZA FAIDA YA BILIONI728 BAADA YA KODI

BENKI YA CRDB YAWEKA REKODI, YATENGENEZA FAIDA YA BILIONI728 BAADA YA KODI

 Na Seif Mangwangi, Arusha

Benki ya CRDB imeanza mwaka 2025 kwa mafanikio makubwa baada ya kurekodi faida baada ya kodi ya Shilingi bilioni 728.6, sawa na ongezeko la asilimia 32.1, huku ikiendelea kupanua huduma zake kimataifa kwa kufungua tawi jipya Dubai katika falme za kiarabu.

Mafanikio hayo yamechangiwa na ukuaji wa huduma za kidijitali, kuongezeka kwa wateja pamoja na uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya kifedha, hatua zinazoifanya Benki hiyo kuendelea kuimarisha nafasi yake kama moja ya taasisi kubwa za kifedha Afrika Mashariki.


Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa 31 wa Wanahisa uliofanyika Leo 16 Mei2026,  katika ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa  AICC, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dkt. Abdulmajid Nsekela, amesema mwaka 2025 ulikuwa  mwaka wa mafanikio makubwa kutokana na utekelezaji madhubuti wa mkakati wa kidijitali pamoja na uwekezaji katika huduma jumuishi za kifedha.

Dkt. Nsekela amesema CRDB imefanikiwa kuwafikia zaidi ya wateja milioni 7.2 kupitia mtandao wake mpana wa huduma unaojumuisha  matawi ya benki hiyo yaliyoko katika nchi za Tanzania, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) pamoja na Ofisi ya Uwakilishi ya Dubai.


Alieleza kuwa mageuzi ya mifumo ya kidijitali yameongeza ufanisi katika utoaji huduma na kurahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha kwa makundi mbalimbali ya wananchi ndani na nje ya Tanzania.

Kwa mujibu wa Dkt. Nsekela, mafanikio hayo yamechangiwa pia na uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya kifedha ambapo Benki hiyo sasa inaongoza kwa kuwa na matawi zaidi ya 261 na mashine za ATM 732 katika maeneo mbalimbali.

Aidha, benki hiyo ina mawakala 38,883 pamoja na vituo vya malipo na manunuzi (POS) 6,607, hatua ambayo imeendelea kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wananchi wengi zaidi.

Dkt Nsekela amesema CRDB inaendelea kujenga uzoefu bora kwa wateja kupitia matumizi ya teknolojia ya kisasa, ubunifu wa huduma za kifedha na dhamira yake ya kubadilisha maisha ya wananchi huku ikichochea maendeleo ya uchumi wa Taifa na ukanda mzima wa Afrika Mashariki.


Katika mkutano huo ulioanza Jana Mei15, 2026 Kwa semina iliyotolea Kwa wanahisa wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa CRDB, Prof. Neema Mori, amewasilisha pendekezo la gawio la Shilingi 90 kwa kila hisa, akieleza kuwa hatua hiyo ni matokeo ya utendaji imara wa Benki kwa mwaka 2025.

Prof. Mori amesema mtaji wa wanahisa umefikia Shilingi trilioni 2.7 huku kiwango cha faida kwa mtaji wa wanahisa (ROAE) kikifikia asilimia 29.5, jambo linaloonyesha uimara wa kifedha wa benki hiyo.


Ameongeza kuwa mafanikio hayo yameongeza imani ya wawekezaji na kuifanya thamani ya hisa ya Benki hiyo kuendelea kuimarika hadi kufikia Shilingi 2,980 mwezi Aprili mwaka huu 2026.

Prof. Mori amewashukuru wanahisa, wateja, washirika wa maendeleo, menejimenti pamoja na wafanyakazi wa CRDB kwa mchango wao mkubwa ulioiwezesha Benki kuendelea kupata mafanikio na kuimarisha nafasi yake katika sekta ya fedha nchini na ukanda wa Afrika Mashariki.





Post a Comment

Previous Post Next Post