
Na Mwandishi wetu
Kama kuna sauti inayozidi kugusa mioyo ya wengi kwenye muziki wa injili kutoka Shinyanga, basi jina la Jesca Simuchile haliwezi kuachwa pembeni.
Kwa muda mrefu mashabiki wake walikuwa wakijiuliza ukimya wake umetokana na nini.
Wapo waliokuwa wakisubiri kuona hatua mpya kutoka kwake, wengine wakitamani kuona video ya wimbo wake uliotikisa wengi wa “Tushikamane”. Sasa majibu yamepatikana!
Jesca Simuchile ambaye anakulia kiroho katika kanisa la International Evangelical Assemblies of God Tanzania Majengo chini ya Askofu David Mabushi, amefunguka kuwa alikuwa jijini Dar es Salaam kwa kazi maalum ya kurekodi video ya album yake kupitia kampuni maarufu ya Hassan Mbangwa Production.
Akizungumza kwa furaha baada ya kurejea Shinyanga, Jesca amesema ukimya wake haukuwa wa kawaida, bali ulikuwa ni muda wa maandalizi ya kazi yenye viwango vya juu ili kuwapa mashabiki wake kile walichokuwa wakikihitaji kwa muda mrefu.
“Wadau wangu walikuwa wanahitaji video kwa muda mrefu. Nimewasikia, na sasa nimeamua kuvunja ukimya rasmi. Hakuna kulala tena,” amesema Jesca huku akionesha matumaini makubwa ya safari yake mpya ya muziki.
Muimbaji huyo amesema tayari ameanza kuandaa kazi nyingine mpya, akionesha wazi kuwa sasa ameamua kuingia rasmi kwenye ushindani wa muziki wa injili kwa nguvu mpya na ubunifu mkubwa zaidi.
Mbali na kipaji chake cha kuimba, Jesca Simuchile pia ni MC anayefanya shughuli mbalimbali za kijamii, sherehe na matukio ya kiserikali pamoja na yasiyo ya kiserikali, jambo linalomfanya kuwa mmoja wa wanawake wanaotumia vipaji vyao kugusa jamii kwa njia tofauti.
Kinachovutia zaidi ni ubunifu wake wa kuanzisha bidhaa maalum zenye nembo ya Tushikamane ikiwemo T-shirts, jezi, tracksuit, kofia, keyholders na bidhaa nyingine mbalimbali.
Kwa mujibu wa Jesca, bidhaa hizo si biashara tu, bali ni sehemu ya kueneza injili na kusaidia huduma yake kufika mbali zaidi.
Jesca hakusita kutoa shukrani zake kwa Mungu kwa kufanikisha safari yake ya kurekodi video hiyo salama, huku akimpongeza Askofu David Mabushi kwa kumuombea na kumtia moyo kila siku.
Pia amemshukuru meneja wake Bwana Osward Jonas Mateng’e pamoja na mashabiki wake wote waliomvumilia katika kipindi cha ukimya wake.
Kwa sasa kazi hiyo ipo mikononi mwa Director Hassan Mbangwa jijini Dar es Salaam kwa hatua za mwisho kabla ya kuachiwa rasmi kupitia mitandao ya kijamii pamoja na mfumo wa Flash.
Kupitia ujumbe wake wenye msingi wa umoja na upendo, Jesca Simuchile anaendelea kuthibitisha kuwa muziki wa injili si burudani pekee, bali ni huduma inayoweza kugusa maisha ya watu wengi na kuleta matumaini mapya kwa jamii.
Wasiliana na Jesca Simuchile 0713 530 707 au 0764 150 795
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254












Post a Comment