Mkuu wa Idara ya Utamaduni, Makongamano na Utalii Taifa wa jumuiya ya shujaa wa maendeleo na ustawi wa jamii Tanzania (SMAUJATA), Shujaa Daniel Kapaya, ameitaka jamii kujenga utaratibu wa kutembelea makumbusho na maeneo ya kihistoria ili kujifunza historia, mila na desturi za Tanzania, hasa katika kipindi hiki ambacho vijana wengi wamekuwa wakitumia muda mwingi kwenye mitandao ya kijamii.
Kapaya ameyasema hayo mapema akiwa kwenye kipindi maalum cha maadhimisho ya Siku ya Makumbusho Duniani kilichorushwa na Redio Faraja FM Stereo mjini Shinyanga, akiwa pamoja na Afisa Utalii wa Manispaa, Bi. Ashura, pamoja na Mwenyekiti wa Idara ya Utamaduni, Makongamano na Utalii Mkoa wa Shinyanga, Mch. Ester.
Akizungumza kwenye kipindi hicho, Kapaya amesema Siku ya Makumbusho Duniani ina umuhimu mkubwa kwa jamii kwani inasaidia kuhifadhi na kurithisha historia kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Amesema kutokana na changamoto za maisha pamoja na matumizi makubwa ya mitandao ya kijamii, vijana wengi wameanza kupoteza muda wa kujifunza historia na tamaduni zao, hali ambayo inaweza kuathiri maadili na utambulisho wa jamii katika siku zijazo.
“Ni muhimu sasa jamii ikaweka utaratibu wa kutembelea makumbusho, hususan wanafunzi wa shule za msingi na sekondari pamoja na wananchi kwa ujumla, ili waweze kujifunza historia ya mambo ya kale na kuthamini urithi wa taifa letu,” amesema Kapaya.
Aidha, ameiomba serikali kuangalia uwezekano wa kujenga majengo ya makumbusho katika mikoa ambayo bado haina huduma hiyo, akisisitiza kuwa kila mkoa nchini una historia, mila na utamaduni wake unaostahili kuhifadhiwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Kwa upande wake, Afisa Utalii wa Manispaa ya Shinyanga, Bi. Ashura, amesema Mkoa wa Shinyanga una vivutio vingi vya utalii vinavyoweza kusaidia kukuza uchumi pamoja na kuhifadhi utamaduni wa wananchi wake.
Akitaja baadhi ya maeneo hayo, amesema ni pamoja na Chibe, Old Shinyanga, Ibadakuli kwenye maji moto, Jambo Zoo, pamoja na Mazingira Center ambayo inahifadhi utamaduni wa Kisukuma kupitia makumbusho ya utamaduni.
Naye Mwenyekiti wa Idara ya Utamaduni Mkoa wa Shinyanga, Mch. Ester, amesema ipo haja kwa wazazi na walezi kutumia fursa ya maadhimisho hayo kuwapeleka vijana katika maeneo ya kihistoria ili waweze kujifunza tamaduni za Kitanzania na kutambua miiko pamoja na maadili ya jamii zao.
“Tukiwafundisha vijana wetu historia na tamaduni zao, tutasaidia kujenga jamii yenye maadili, heshima na uzalendo kwa taifa lao,” amesema Mch. Ester.
Maadhimisho ya Siku ya Makumbusho Duniani mwaka 2026 yanaongozwa na kauli mbiu isemayo; “Makumbusho Inaunganisha Dunia Iliyogawanyika” (Museums Unite a Divided World).
Mkuu wa Idara ya Utamaduni, Makongamano na Utalii Taifa, Shujaa Daniel Kapaya, akizungumza kwenye kipindi.

SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254











Post a Comment