" MAZISHI YA BOAZ MARTINE KUFANYIKA KESHO MWAWAZA, MSIBA UPO KITANGILI SHINYANGA MJINI

Top News

MAZISHI YA BOAZ MARTINE KUFANYIKA KESHO MWAWAZA, MSIBA UPO KITANGILI SHINYANGA MJINI

 Mazishi ya aliyekuwa Mpiga Picha wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, marehemu Boaz Martine, yanatarajiwa kufanyika kesho Alhamisi Mei 21, 2026 katika makaburi ya familia yaliyopo Mwawaza, Manispaa ya Shinyanga.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Utawala na Rasilimali Watu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, David Lyamongi, ibada ya kumuombea marehemu itaongozwa na Mashahidi wa Yehova kuanzia saa 7:00 mchana nyumbani kwa marehemu nyuma ya Ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Kitangili, Manispaa ya Shinyanga.

Baada ya ibada na salamu za rambirambi, mwili wa marehemu utapelekwa katika makaburi ya familia yaliyopo Mwawaza kwa ajili ya mazishi yatakayoanza majira ya saa 9:00 alasiri.

Marehemu Boaz Martine alifariki dunia Mei 19, 2026 kufuatia ajali ya barabarani iliyotokea katika eneo la Samuye mkoani Shinyanga, ajali iliyohusisha gari lililokuwa limebeba waandishi wa habari pamoja na watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.

Akizungumza na waandishi wa habari Mei 20, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga SACP Janeth Magomi alisema ajali hiyo ilisababishwa na uzembe wa dereva wa gari aina ya Toyota Harrier aliyekuwa akijaribu kulipita gari lililokuwa mbele yake bila tahadhari.

Mbali na marehemu Boaz Martine, watu saba walijeruhiwa katika ajali hiyo ambao ni Frank Mshana wa ITV/Radio One, Johnson James, Koplo Swahiba Msangi, Neema Madono (36), Rehema Edson (45), Shadia Omari (32) pamoja na dereva wa gari la Land Cruiser Laurence Peter (34).

Majeruhi hao wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga na wengine katika Hospitali ya Rufaa Bugando Jijini Mwanza.

MPIGA PICHA WA OFISI YA MKUU WA MKOA WA SHINYANGA AFARIKI DUNIA KATIKA AJALI, WENGINE 7 WAJERUHIWA AKIWEMO MWANDISHI WA HABARI WA ITV

 

Post a Comment

Previous Post Next Post