" MWENYEKITI WA MPITO STAND UNITED AACHIA NGAZI KULINDA HESHIMA

MWENYEKITI WA MPITO STAND UNITED AACHIA NGAZI KULINDA HESHIMA

 

Timu ya Stand United imeingia katika mabadiliko mapya ya kiuongozi baada ya Mwenyekiti wake wa mpito, Issa Mbaraka, kutangaza kujiuzulu rasmi wadhifa huo kufuatia changamoto za ndani zilizokuwa zikiikumba timu hiyo.

Akizungumza na vyombo vya habari Mei Mosi, 2026 mkoani Shinyanga, Mbaraka amesema uamuzi wake umetokana na tofauti kubwa za kimtazamo kati yake na baadhi ya viongozi wenzake, hali iliyokuwa ikiathiri ufanisi wa majukumu yake pamoja na maendeleo ya timu.

Ameeleza kuwa alichukua uamuzi huo kwa nia njema ya kuinusuru Stand United, ili kutoa nafasi kwa wengine kuendelea kuiongoza kwa mtazamo wanaouona unafaa zaidi.

Mbaraka amesema aliteuliwa kushika nafasi hiyo mnamo Novemba 2025 na wadau wa timu, kwa lengo la kuirejesha katika ushindani mzuri baada ya kuwa katika kipindi kigumu cha matokeo yasiyoridhisha.

Aidha, amebainisha kuwa licha ya jitihada zake za kuiboresha timu na kuanza kupata matokeo chanya, bado alikumbana na changamoto ya kukosekana kwa ushirikiano kutoka kwa baadhi ya viongozi, jambo lililoathiri mwelekeo wa uongozi.

“Leo Mei Mosi, 2026 natangaza rasmi kujiuzulu nafasi yangu na sitahusika tena na usimamizi wa timu ya Stand United, kwa kuwa mtazamo wangu wa uongozi unatofautiana na viongozi wenzangu, hali inayoniwekea vikwazo katika utekelezaji wa majukumu yangu,” amesema Mbaraka.

Ameongeza kuwa aliona ni vyema kuwaachia wengine waendelee na mfumo wao wa uendeshaji, huku yeye akilenga kulinda heshima yake katika jamii kutokana na hali iliyokuwa ikiendelea ndani ya timu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Shinyanga, Said ManKilingo, amesema amepokea taarifa hizo kupitia vyombo vya habari na kumshauri Mbaraka kuwasilisha rasmi barua ya kujiuzulu ili kukamilisha taratibu.

ManKilingo ameongeza kuwa kama angepata nafasi ya kuzungumza naye kabla ya kufikia uamuzi huo, angeweza kumshauri na kusaidia kutafuta suluhu ya changamoto zilizokuwa zikikabili uongozi wa timu hiyo.

Naye Mjumbe wa mkutano mkuu TFF kutoka Mkoa wa Shinyanga  Azan Said Mufti amesema kuisaidia timu ya Stand United ni kutokana na kila mtu alivyojaliwa na namna ambavyo anapata msukumo kutoka ndani ya moyo wake na hakuna mtu anaye lazimishwa isipokuwa ni kuipenda timu na kuisaidia ili ipige hatua huku akibainisha kuwa hana taarifa za Mwenyekiti wa mpito wa timu hiyo kujiuzulu.

SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment

Previous Post Next Post