" POLISI WAWASHIKILIA WANNE KWA TUHUMA ZA MAUAJI VIKAWE

POLISI WAWASHIKILIA WANNE KWA TUHUMA ZA MAUAJI VIKAWE




JESHI la Polisi Mkoa wa Pwani linawashikilia watuhumiwa wanne kwa tuhuma za kuhusika katika tukio la mauaji ya watu watatu na kujeruhi watu 14 waliokuwa wakidaiwa kwenda kuvunja nyumba zao Mei 6, 2026 katika eneo la Vikawe, Kibaha mkoani humo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase, akizungumza kuhusu maendeleo ya uchunguzi wa tukio hilo, amesema kuwa Mei 14, 2026 jeshi hilo lilifanya operesheni ya upelelezi kuhusiana na mgogoro huo wa ardhi na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao.

Amewataja watuhumiwa waliokamatwa kuwa ni Mussa Chununu Tembo (34), kuli mkazi wa Vikawe, Walter Urassa (33), fundi ujenzi mkazi wa Vikawe, Jackson Kilundwa (31), fundi ujenzi mkazi wa Vikawe pamoja na David Erick (26), mkazi wa Vikawe.

Aidha, Kamanda Morcase amesema majeruhi 13 waliokuwa wakipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Tumbi na majeruhi mmoja aliyekuwa akitibiwa Hospitali ya Muhas Mloganzila walihojiwa baada ya kumaliza matibabu na kupewa dhamana, isipokuwa majeruhi saba ambao bado wanashikiliwa.

Amefafanua kuwa majeruhi hao saba bado wanashikiliwa katika Kituo cha Polisi Kibaha wakisubiri kukamilika kwa taratibu za dhamana.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani limetoa rai kwa wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi na badala yake kutoa ushirikiano kwa vyombo vya ulinzi na usalama kwa kutoa taarifa kuhusu wahalifu na vitendo vya uhalifu vinavyotokea katika maeneo yao.

Post a Comment

Previous Post Next Post