" STELLA IBENGWE: SERIKALI IENDELEE KUCHUKUA HATUA KALI DHIDI YA WASAMBAZAJI WA HABARI ZA UONGO MTANDAONI

STELLA IBENGWE: SERIKALI IENDELEE KUCHUKUA HATUA KALI DHIDI YA WASAMBAZAJI WA HABARI ZA UONGO MTANDAONI

 

Na Mapuli Kitina Misalaba

Mwandishi wa habari kutoka Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga (Shinyanga Press Club)SPC, Stella Ibengwe, amesema maadhimisho ya World Press Freedom Day ni fursa muhimu kwa wanahabari kujikumbusha wajibu wao wa kutekeleza majukumu kwa weledi na kuzingatia maadili ya taaluma.

Ibengwe amesema siku hiyo ina umuhimu mkubwa kwa waandishi wa habari kwani inawakumbusha wajibu wao wa kuhakikisha wanaripoti habari sahihi, zenye uwiano na zinazozingatia maadili ya uandishi wa habari.

Ameeleza kuwa kuongezeka kwa matumizi ya mitandao ya kijamii kumechangia kusambaa kwa taarifa zisizo sahihi, akibainisha kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakijichukulia jukumu la kuripoti matukio bila kufuata misingi ya taaluma hiyo.

“Kuna tofauti kati ya mwandishi wa habari mtaalamu na mtu wa kawaida anayerekodi tukio na kusambaza bila kuthibitisha taarifa. Hali hii imekuwa ikisababisha kusambaa kwa habari zisizo sahihi na wakati mwingine kuleta taharuki katika jamii,” amesema Ibengwe.

Ameongeza kuwa mwandishi wa habari mtaalamu hawezi kuripoti habari zinazoweza kusababisha taharuki kwa jamii, badala yake huzingatia ukweli, usahihi na maadili ya kazi yake.

Aidha, ameiomba serikali kuendelea kuchukua hatua kali dhidi ya watu wanaosambaza taarifa za uongo kwenye mitandao ya kijamii, akisema vitendo hivyo vinaweza kuleta athari kubwa kwa jamii na taifa kwa ujumla.

“Serikali iendelee kuchukua hatua kwa wale wanaosambaza habari za uongo zinazoweza kusababisha mtafaruku na kuvuruga utulivu wa jamii,” amesisitiza.

Pia amewataka wadau mbalimbali kuendelea kushirikiana na vyombo vya habari ili kuhakikisha taarifa sahihi zinawafikia wananchi kwa wakati na kwa usahihi, akieleza kuwa ushirikiano huo ni muhimu katika kuleta maendeleo ya taifa.

“Ni muhimu kwa wadau kuendelea kutoa ushirikiano kwa waandishi wa habari ili tuweze kutimiza jukumu letu la kuhabarisha jamii kwa kina na kwa usahihi,” amesema.

Ibengwe amesisitiza kuwa lengo la waandishi wa habari ni moja, ambalo ni kuchangia maendeleo ya nchi kupitia utoaji wa taarifa sahihi na zenye manufaa kwa jamii.

SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment

Previous Post Next Post