" ​"TUSIGOMBANE KWA SABABU YA ARDHI" - NAIBU WAZIRI MMUYA AWASIHI WANANCHI WA ZEZE KULINDA AMANI

​"TUSIGOMBANE KWA SABABU YA ARDHI" - NAIBU WAZIRI MMUYA AWASIHI WANANCHI WA ZEZE KULINDA AMANI


Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Mmuya, ametoa wito kwa wananchi wa Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, kutatua migogoro ya ardhi kwa njia ya mazungumzo na amani badala ya kuchukua sheria mkononi.Mhe. Mmuya ametoa kauli hiyo Mei 17, 2026, wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Zeze ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kusikiliza na kutatua kero za ardhi wilayani humo.Akihutubia mamia ya wananchi waliojitokeza, Mhe. Mmuya amesisitiza umuhimu wa kulinda amani ya nchi, akibainisha kuwa ardhi haiongezeki (haitanuki) wakati idadi ya watu inazidi kuongezeka, hali inayoweza kuleta madhara makubwa iwapo migogoro haitashughulikiwa kwa hekima."Tutatue (migogoro) kwa kukaa na kuongea bila kujichukulia sheria mkononi. Nchi hii ina amani na tumeirithi kwetu, tusigombane kwa sababu ya ardhi. Ardhi ni yetu, ardhi haitanuki... sisi watu tunaongezeka, tukianza kugombana itafika muda watu tutapata madhara," amesema Naibu Waziri Mhe. Kaspar Mmuya.Aidha, akijibu kero ya wananchi wa Zeze walioomba kuongezewa ardhi kwa ajili ya kilimo, Naibu Waziri ameweka wazi kuwa taratibu za kisheria lazima zifuatwe ambapo amefafanua kuwa ardhi yote nchini ipo chini ya uangalizi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwamba viongozi wengine kama Mbunge au Mkuu wa Wilaya hawana mamlaka ya kugawa ardhi bila kufuata mchakato rasmi.Mhe. Mmuya amemuagiza Mbunge wa eneo hilo, kwa niaba ya wananchi, kuanzisha mchakato rasmi wa maombi ya ardhi ya ziada, ambayo yatafanyiwa tathmini na wataalamu kabla ya kutolewa kwa uamuzi wa mwisho.Ziara hii ya Mhe. Mmuya ni muendelezo wa utekelezaji wa maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, anayeitaka wizara hiyo kuwafuata wananchi kule waliko ili kumaliza kero za ardhi ambazo zimekuwa zikihusisha maeneo mbalimbali nchini.





 

Post a Comment

Previous Post Next Post