Na John Walter-Babati, Manyara

Jioni ya kawaida mjini Babati, kundi la wanaume lilikuwa limekusanyika kuangalia mpira.

Vicheko na kelele za shangwe vilitawala hewani, hadi pale ghafla hali ilipobadilika.

Mwanaume mmoja alisimama kwa taharuki, akapiga kelele kwa sauti ya hofu: “Nyeti zangu zimepotea!”

Ndani ya sekunde chache, furaha ilitoweka.

Watu wakasogea kwa taharuki, wengine wakaanza kukimbia, huku macho yakianza kumtafuta mtu wa kulaumiwa.

Kilichoanza kama dai la mtu mmoja kiligeuka kuwa hofu ya pamoja—hofu iliyosambaa kwa kasi kama moto wa nyika.

Matukio kama hayo yameendelea kujirudia katika maeneo mbalimbali nchini, yakichochewa na taarifa za uzushi zinazosambaa mitandaoni kuwa mwanaume akiguswa begani hupoteza sehemu zake za siri.

Kwa mujibu wa David Misime,msemaji wa jeshi la polisi nchini, ndani ya siku nne pekee, watu saba walipoteza maisha huku wengine wakijeruhiwa baada ya wananchi kujichukulia sheria mkononi dhidi ya watu waliotuhumiwa kuhusika na vitendo hivyo.

Anasema uchunguzi uliofanywa umebaini kuwa madai hayo hayana ukweli wowote, kwani waliodai kupoteza sehemu zao walikutwa nazo, jambo linaloonyesha wazi kuwa hofu hiyo inachochewa na imani potofu na uvumi usio na msingi.

Wakati mamlaka zikijaribu kuzima taharuki hiyo, taarifa hizo zinaendelea kusambaa kwa kasi kupitia mitandao ya kijamii, zikiwafikia watu wengi ndani ya muda mfupi.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, ameonya kuwa taarifa hizo ni za upotoshaji na zinachochea hofu isiyo ya lazima katika jamii, akizitaka jamii kuzipuuza na kutozieneza.

Lakini kwa wananchi kama Mbaraka Sungi, tukio alilolishuhudia bado linamkaa akilini.

Anasema siku hiyo alipokuwa akiangalia mpira, mwanaume mmoja alisimama ghafla na kuanza kupiga kelele kuwa amepoteza nyeti zake baada ya kushikwa bega.

Watu walimzunguka kwa mshangao na hofu, huku hali ya sintofahamu ikitawala eneo hilo. “Ilikuwa hali ya kutisha sana,” anasema, akiongeza kuwa baada ya tukio hilo, wanaume wengi walianza kuishi kwa hofu, wakihofia hata kuguswa na watu wengine.

Hofu hiyo inaungwa mkono na kauli za baadhi ya wananchi wanaoona kuwa uvumi huo umevuka mipaka na kuwa tishio kwa usalama wa jamii.

Lucas Mondu anasema si jambo la kulifumbia macho, akisisitiza kuwa wanaosambaza propaganda hizo wanapaswa kuchukuliwa hatua kali.

Naye Rose Njate anasema alishuhudia taarifa hizo zikisambaa kwa kasi mitandaoni, hali iliyochochea taharuki na hofu miongoni mwa wananchi.

Kwa mtazamo wa kitaalamu wa kidini, Clemence Matwiga anaeleza kuwa imani potofu huota mizizi katika ukosefu wa elimu sahihi ya kiimani na uelewa mdogo wa mambo ya msingi.

Anasema jamii inapokosa maarifa sahihi, huwa rahisi kuamini jambo lolote linaloibua hofu, hata kama halina ushahidi wa ukweli.

Hali hiyo, anaonya, inaweza kusababisha watu kuchukua hatua za haraka na za hatari dhidi ya wenzao.

Mtazamo huo unaungwa mkono na viongozi wa kimila, akiwemo Chifu Dodo Zuberi Sige Chifu wa Wagorowa , ambaye anasema baadhi ya watu wameanza kupotosha mila na kuziingiza katika vitendo visivyo na msingi.

Anasisitiza kuwa mila halisi hazihusiani na ukatili au mauaji, bali kinachoonekana sasa ni kupotoka kwa maadili na matumizi mabaya ya imani za jadi.

Katika muktadha huu, matukio ya kushambuliwa na kuuawa kwa watu wanaotuhumiwa kuhusika na vitendo hivyo yanaibua taswira ya jamii inayosukumwa na hofu kuliko ukweli.

Uvumi unapoanza, huzalisha hofu; hofu huzalisha hasira; na hasira, mara nyingi, huishia katika vurugu na mauaji ya watu wasio na hatia.

Jeshi la Polisi pia limeeleza kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakisambaza taarifa hizo kwa makusudi, hata kwa njia ya vichekesho, ili kuvutia wafuasi katika mitandao ya kijamii.

Kitendo hicho, kwa mujibu wa mamlaka, si tu kinachochea hofu bali pia kinachangia moja kwa moja madhara yanayoikumba jamii.

Kadri teknolojia inavyorahisisha mawasiliano, ndivyo pia inavyorahisisha kusambaa kwa taarifa za uongo.

Katika mazingira haya, mstari kati ya ukweli na uzushi unazidi kuwa mwembamba, na madhara yake yanabebwa na wananchi wa kawaida.

Swali linalobaki ni je, jamii itaendelea kuamini kila kinachosikika bila kuthibitisha, au itachagua kusimama upande wa ukweli na kulinda maisha ya watu?

SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254