" VIJANA WA KIZAZI CHA GEN Z WATAKIWA KUWA WALINZI WA AMANI YA TAIFA

VIJANA WA KIZAZI CHA GEN Z WATAKIWA KUWA WALINZI WA AMANI YA TAIFA

 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Halid Mwinyi, amewasihi vijana wa kizazi cha sasa maarufu kama Gen Z kuendelea kuilinda amani ya nchi kama dhima yao kuu kwa ustawi wa taifa.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam wakati wa kilele cha mashindano ya mpira wa miguu yaliyoandaliwa na Wilaya ya Kinondoni, Mwinyi alisisitiza kuwa vijana wanapaswa kupendana na kushikamana ili kuhakikisha Tanzania inabaki kuwa kisiwa cha utulivu.

Alikumbushia kauli ya vijana waliyotoa mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan hivi karibuni jijini Dodoma walipoahidi kutorejea tena katika makosa ya nyuma yaliyojiri mwezi Oktoba, huku akitoa onyo kali kwa watu wanaojaribu kuwafarakanisha vijana na kiongozi wao mkuu wa nchi.

Mwinyi alieleza kuwa umoja na amani ndivyo vitu muhimu zaidi kwa maendeleo ya taifa lolote duniani, hivyo wakazi wa Dar es Salaam na Watanzania kwa ujumla wanapaswa kumuunga mkono Rais Samia katika jitihada zake za kuleta maridhiano na maendeleo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Kinondoni, Abdulrahman Abdallah Kassim, alibainisha kuwa mashindano hayo yaliyodumu kwa mwezi mmoja yalikuwa na lengo la kuonesha namna wananchi, hususan vijana, wanavyoendelea kuwa na imani na CCM na serikali yake.

Alituma salamu za dhati kwa Rais akimhakikishia kuwa vijana wanampenda na wapo tayari kumlinda na kusimamia amani ya nchi wakati wote ili kuzuia mifarakano inayoweza kuchelewesha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Katika kilele cha mashindano hayo yaliyofana, mshindi wa kwanza alizawadiwa kombe pamoja na kitita cha shilingi milioni tatu, huku mshindi wa pili akipata shilingi milioni 1.4 na mshindi wa tatu akiondoka na shilingi milioni moja.

Aidha, Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Mohamed Kawaida, kupitia kwa Katibu Mkuu Mwinyi, aliongeza zawadi ya shilingi laki tatu kwa kila timu iliyoshika nafasi ya kwanza, pili, na tatu kama motisha kwa vijana hao walioonyesha nidhamu na mshikamano wakati wote wa michuano.

Tukio hilo limeonekana kuwa jukwaa muhimu la michezo linalotumika kuhimiza uzalendo, kulinda mali za umma, na kuhakikisha kuwa vijana wanatumia nguvu zao katika shughuli zinazojenga badala ya kushiriki katika vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama wa taifa.

Post a Comment

Previous Post Next Post