" WAJASIRIAMALI DODOMA WAMSIMAMISHA RAIS SAMIA, WASEMA “NEVER AGAIN,” WAOMBA UWEZESHAJI ZAIDI

WAJASIRIAMALI DODOMA WAMSIMAMISHA RAIS SAMIA, WASEMA “NEVER AGAIN,” WAOMBA UWEZESHAJI ZAIDI

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na wananchi wa maeneo mbalimbali ya Jiji la Dodoma pembezoni mwa Uwanja wa Ndege wa Dodoma kabla ya kuelekea Jij itini Dar es Salaam tarehe 08 Mei, 2026.

***

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka vijana nchini kulinda amani na kutokubali kutumika katika vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama na taswira ya nchi. 

Kauli hiyo ameitoa Mei 8,2026 jirani na Uwanja wa Ndege wa Dodoma akiwa njiani kuelekea Dar es Salaam, baada ya kusimamishwa na maelfu ya wakazi wa mkoa huo wakiwemo vijana, maafisa usafirishaji, machinga, mamalishe na babalishe. 

Wananchi hao walijitokeza wakiwa wamevaa fulana na mabango yenye ujumbe wa “Never Again” yaani yasijirudie, wakirejea vurugu za uvunjifu wa amani zilizotokea Oktoba 29, 2025, wakati na baada ya uchaguzi mkuu uliopita.

Akiupokea ujumbe huo kwa faraja, Rais Dkt. Samia amesisitiza kuwa matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea huko nyuma hayakuwa mema kwa yeyote na yamelitia doa Taifa, hivyo hayapaswi kupewa tena nafasi katika jamii. 

Amewaomba vijana kuelimishana katika vijiwe na maeneo yao ya kazi ili wasikubali kutiwa maneno ya kuharibu usalama wa nchi, huku akikumbusha kuwa aliamua kutoa msamaha kwa waliohusika awali baada ya kuona wengi waliingia kwa mkumbo na walikuwa wameshajifunza. Rais amewataka vijana kuwa walinzi wa amani na kulindana wenyewe kwa wenyewe ili kulinda taswira ya nchi na maisha ya wananchi kwa ujumla.

Katika upande wa uwezeshaji wa kiuchumi, Rais Samia amewahakikishia wajasiriamali hao kuwa Serikali imeanza hatua za kusimamia utoaji wa mikopo kupitia taasisi nyingi zaidi za kifedha ili kuongeza wigo wa upatikanaji wa mitaji. 

Amekiri kuwa mahitaji ya mikopo ni makubwa na kuahidi kuongeza rasilimali kadiri uchumi unavyoruhusu, ikiwa ni pamoja na kufanyia kazi ombi la mamalishe na babalishe la kuboresha masharti ya mikopo ya makundi maalum ili kunufaisha watu wa kipato cha chini. 

Aidha, ameelekeza kufanyika kwa tathmini ya kuanzisha soko lingine la wafanyabiashara wadogo pembezoni mwa Soko la Machinga Complex ili kukuza fursa na kupunguza msongamano.

Wajasiriamali hao kupitia wawakilishi wao wameishukuru Serikali kwa maboresho yaliyofanyika ikiwemo ujenzi wa Soko la Machinga Complex ambalo limekuwa mfano bora wa upangaji wa biashara ndogondogo. 

Pamoja na shukrani hizo, wameomba kuimarishwa kwa huduma za usafiri wa daladala kufika sokoni, usimamizi endelevu wa maeneo rasmi ya biashara, na kuahidi kupitia maafisa usafirishaji kuwa wataendelea kushirikiana na mamlaka kuzuia matumizi mabaya ya vyombo vya moto kufanya fujo. 

Rais amehitimisha kwa kuwaahidi kurejea Dodoma baada ya mwezi mmoja kwa ajili ya ziara maalum ya kusikiliza kero zao na amewaelekeza viongozi wa mkoa kuanza kufanyia kazi hoja zote zilizowasilishwa.

SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment

Previous Post Next Post