" WANANCHI WA KILWA MASOKO WAIPONGEZA REA KWA MAFUNZO YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA

WANANCHI WA KILWA MASOKO WAIPONGEZA REA KWA MAFUNZO YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA

Wananchi wa Wilaya ya Kilwa Masoko mkoani Lindi, wametoa pongezi na shukrani kwa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kuendelea kusambaza teknolojia na kutoa mafunzo ya nishati safi ya kupikia wilayani humo.

Shukrani hizo zilitolewa hivi karibuni wakati wa kongamano maalum la Watu wenye changamoto ya kusikia (Viziwi), lililofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kilwa Masoko mkoani Lindi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wakazi wa eneo hilo walieleza jinsi nishati safi ilivyobadilisha maisha yao na kuondokana na adha ya matumizi ya kuni na mkaa.

Mmoja wa wakazi hao, Bi. Hawa Ally, alisema matumizi ya kuni hapo awali yalikuwa yanachangia ugumu wa utayarishaji wa chakula, hasa nyakati za masika kutokana na kuni kuwa mbichi.

"Kuni na mkaa zilikuwa gharama kubwa kwangu. Wakati wa mvua, ilikuwa inanilazimu kutumia muda mwingi kuwasha nishati hizo ambazo pia zilipatikana kwa shida," alisema Bi. Hawa. Naye mwananchi mwingine, Bi. Mwanahamisi Juma, aliongeza kuwa jiko la gesi limerahisisha maisha ya familia yake, hasa pale anapolazimika kumtengenezea mtoto chakula nyakati za usiku.

Hata hivyo, Bi. Mwanahamisi alitoa wito kwa Serikali kuangalia uwezekano wa kupunguza gharama za gesi ili wananchi wengi zaidi waweze kumudu.

Kwa upande wake, Mtaalam wa Nishati na Jinsia kutoka REA, Dkt. Joseph Sambali, alisisitiza kuwa matumizi ya nishati safi ni muhimu kwa afya, uhifadhi wa mazingira, na ukuzaji wa uchumi wa muda mrefu.

Dkt. Sambali alitaja vyanzo vya nishati safi kuwa ni pamoja na umeme, gesi ya kupikia (LPG), nishati ya jua, na upepo, ambavyo vinachukua nafasi ya nishati asilia zisizo safi na salama.

"Majiko ya nishati safi hayatoi masizi. Huleta mazingira safi, ya heshima, na ya starehe nyumbani," alisema Dkt. Sambali.

Serikali kwa sasa inatekeleza Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia, ukiwa na lengo la kuhakikisha asilimia 80 ya wananchi wanatumia nishati bora ifikapo mwaka 2034.

Post a Comment

Previous Post Next Post