" DIRISHA LA TUZO LAFUNGULIWA, WATAFITI WATAKIWA KUONESHA UBORA WAO

DIRISHA LA TUZO LAFUNGULIWA, WATAFITI WATAKIWA KUONESHA UBORA WAO

Na.Alex Sonna -DODOMA

Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Prof Adolf Mkenda amezindua dirisha la maombi ya Tuzo za nne za Utafiti kwa Watafiti Waliochapisha Matokeo ya Tafiti zao kwenye Majarida yenye Hadhi ya Juu Kimataifa.

Dirisha hilo litakuwa wazi kuanzia Juni 19 hadi Oktoba 31, 2026 na litatoa fursa kwa watafiti wenye sifa kuwasilisha maombi yao kwa ajili ya kutambuliwa na kupewa tuzo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo Juni 18, 2026 jijini Dodoma, Profesa Mkenda amesema tuzo hizo zitahusisha nyanja nne muhimu za utafiti ambazo ni Sayansi Asilia na Hisabati, Afya na Sayansi Shirikishi, Sayansi za Wanyama na Kilimo, pamoja na Uhandisi na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.

Amesema lengo la tuzo hizo ni kuhamasisha watafiti nchini kufanya tafiti zenye ubora wa hali ya juu, kuongeza idadi ya machapisho ya kisayansi yanayotambulika kimataifa, na kuimarisha mchango wa tafiti katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya Tanzania.

 "Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa watafiti na wabunifu ili kuhakikisha matokeo ya tafiti yanatumika kutatua changamoto mbalimbali za maendeleo na kuongeza ushindani wa taifa katika nyanja za sayansi, teknolojia na ubunifu."amesema Prof.Mkenda

Amesema juhudi hizo zinaendana na azma ya Serikali ya kujenga uchumi unaotegemea maarifa, utafiti na matumizi ya teknolojia katika kuongeza tija kwenye sekta mbalimbali za uzalishaji na utoaji huduma.

Aidha, Waziri Mkenda amewahimiza watafiti wenye machapisho katika majarida yenye hadhi ya juu kimataifa kujitokeza kwa wingi na kuwasilisha maombi yao ndani ya muda uliopangwa ili kupata fursa ya kutambuliwa kwa mchango wao katika kukuza maarifa, uvumbuzi na maendeleo ya taifa.

Post a Comment

Previous Post Next Post