" DKT. KIJAJI AANIKA MIKAKATI ENDELEVU YA KUKUZA SEKTA YA UTALII

DKT. KIJAJI AANIKA MIKAKATI ENDELEVU YA KUKUZA SEKTA YA UTALII

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) ameeleza mikakati mbalimbali inayotekelezwa na Serikali kwa lengo la kuendelea kukuza Sekta ya Utalii nchini, ikiwa ni pamoja na kutangaza vivutio vya utalii katika masoko mapya ya kimataifa, kuimarisha miundombinu ya utalii na kupanua wigo wa bidhaa za utalii.Akizungumza katika mahojiano maalumu na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) yaliyofanyika ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Arusha mara baada ya kushiriki uzinduzi wa matokeo ya Sensa ya Wanyamapori Tanzania, Dkt. Kijaji alisema Wizara yake imeanza kutekeleza mkakati maalumu wa kuvitangaza vivutio vya utalii vya Tanzania katika masoko ya nchi za Mashariki ya Mbali ili kuvutia watalii wengi zaidi kutoka maeneo hayo.Alisema mkakati huo ni sehemu ya juhudi pana za kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa Kitovu cha Utalii barani Afrika na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika maendeleo ya uchumi wa taifa.“Lengo letu ni kuongeza idadi ya watalii wa ndani na wa kimataifa, kuongeza mapato ya fedha za kigeni na kufungua fursa zaidi za ajira kwa Watanzania."Tayari jitihada za awali za kutangaza vivutio vyetu katika masoko ya Mashariki ya Mbali zimeanza kuzaa matunda, kwani tumeshuhudia ongezeko la watalii kutoka nchi hizo, hususan China,” alisema Dkt. Kijaji.Aliongeza kuwa Serikali imejipanga kupanua mazao ya utalii kwa kuwekeza katika bidhaa nyingine za utalii mbali na utalii wa wanyamapori ambao kwa muda mrefu umekuwa ukiongoza nchini.“Kwa sasa tunaelekeza nguvu kubwa katika kuendeleza na kutangaza vivutio vingine vya utalii vinavyopatikana Tanzania, ikiwemo utalii wa misitu, utalii wa kiikolojia, utalii wa utamaduni na vivutio vingine vya kipekee vinavyopatikana katika maeneo mbalimbali ya nchi,” alifafanua.Kwa mujibu wa Dkt Kijaji,  watalii wengi wameanza kuonesha hamasa ya kutembelea maeneo ya misitu yanayosimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa ajili ya shughuli za utalii wa kiikolojia.Alisema ili kuboresha eneo hilo, Wizara kwa kushirikiana na TFS inaendelea kuboresha miundombinu muhimu katika hifadhi za misitu ili kuhakikisha wageni wanapata huduma bora zinazokidhi viwango vya kimataifa.“Tunafanya maboresho makubwa ya miundombinu katika hifadhi mbalimbali za misitu na wakati huo huo tunahamasisha uwekezaji wa sekta binafsi katika huduma za malazi, usafiri na huduma nyingine za utalii,” alisema.Dkt. Kijaji alibainisha kuwa Serikali pia imeweka mkazo katika kuendeleza vivutio vya utalii vilivyopo katika kanda zote za utalii nchini badala ya kutegemea zaidi Kanda ya Kaskazini pekee.“Kwa muda mrefu Sekta ya Utalii imejikita zaidi katika Kanda ya Kaskazini, lakini sasa tumedhamiria kukuza na kutangaza vivutio vilivyopo katika kanda zote za utalii nchini ili kuongeza mchango wake katika uchumi wa taifa,” alisema.Alimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa zaidi ya Sh. bilioni 300 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya utalii katika Kanda ya Kusini, hatua ambayo imechangia kuimarika kwa huduma na kuongeza mvuto wa vivutio vya utalii katika eneo hilo.Alisema moja ya matokeo ya uwekezaji huo ni ujenzi wa viwanja vya ndege vya kisasa katika Hifadhi za Taifa za Nyerere na Ruaha, ambavyo vimeongeza urahisi wa kufika katika maeneo hayo na kuvutia watalii zaidi.Katika hatua nyingine, Waziri alisema Wizara inaendelea kuwaunganisha wadau wa Sekta ya Utalii nchini na wenzao wa kimataifa ili kuongeza kasi ya kutangaza vivutio vya Tanzania katika masoko ya nje.

SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

 

Post a Comment

Previous Post Next Post