" ISENENGEJA FC YAIONDOA MWAKITOLYO NO. 6 KWA PENATI 3-1, NIACHEKONA CUP 2026

ISENENGEJA FC YAIONDOA MWAKITOLYO NO. 6 KWA PENATI 3-1, NIACHEKONA CUP 2026

Na Mapuli Kitina Misalaba

Timu ya Isenengeja FC kutoka Mkoa wa Mwanza imefanikiwa kutinga hatua ya timu 12 bora za mashindano ya NIACHEKONA CUP 2026 baada ya kuibuka na ushindi wa mikwaju ya penati 3-1 dhidi ya Mwakitolyo No. 6 katika mchezo wa marudiano uliochezwa katika Uwanja wa Mwabenda, Kata ya Solwa, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.

Katika mchezo wa kwanza, Isenengeja FC iliibuka na ushindi wa bao 1-0, huku mchezo wa leo Juni 5, 2026 ukiwashuhudia Mwakitolyo No. 6 wakijibu mapigo kwa ushindi wa bao 1-0 ndani ya dakika 90 za kawaida.

Matokeo hayo yaliifanya jumla ya mabao katika michezo yote miwili kuwa sare ya 1-1, hali iliyolazimu mshindi kupatikana kwa mikwaju ya penati kwa mujibu wa kanuni za mashindano hayo.

Katika hatua hiyo ya maamuzi, Isenengeja FC walionesha umakini mkubwa na kufanikiwa kushinda kwa penati 3-1, ushindi uliowapa tiketi ya kusonga mbele huku safari ya Mwakitolyo No. 6 katika mashindano hayo ikifikia tamati.

Baada ya mchezo huo, viongozi wa Mwakitolyo No. 6 walimshukuru mwandaaji wa mashindano hayo kwa kuwapa nafasi ya kushiriki NIACHEKONA CUP 2026, huku wakitoa pole kwa mashabiki wao waliokuwa na matumaini ya kuwaona wakifika hatua za mwisho za mashindano hayo.

Kwa upande wa Isenengeja FC, ushindi huo unaifanya timu hiyo kukutana na Kimandaguli FC katika hatua inayofuata ya mashindano hayo, baada ya Kimandaguli FC kufuzu jana kwa ushindi wa penati dhidi ya Kashishi FC.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Katibu wa Kamati ya Mashindano, Sambayi Jilya, ametangaza kuwa mchezo wa kesho utawakutanisha Bulige FC kutoka Wilaya ya Kahama na Sangu FC kutoka Mkoa wa Mwanza katika pambano linalotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.

Ameendelea kuwakaribisha wananchi, wadau wa michezo na mashabiki wa soka kujitokeza kwa wingi katika Uwanja wa Mwabenda ili kuendelea kushuhudia vipaji vya vijana na burudani ya michezo inayotolewa kupitia mashindano hayo.

Mashindano ya NIACHEKONA CUP 2026 yameandaliwa na mdau wa michezo Paul Daud Augustino maarufu MC NIACHEKONA kwa ufadhili wa shirika la Lushu Foundation, yakiwa na lengo la kuibua vipaji vya vijana, kuimarisha amani na kukuza michezo katika jamii.

Kwa mawasiliano ya huduma za ushereheshaji wa shughuli mbalimbali, matangazo na matukio ya kijamii, MC NIACHEKONA anapatikana kupitia namba 0757 267 738.

Kikosi cha Isenengeja FC.


 

Post a Comment

Previous Post Next Post