" JANGA LA KIDIJITI:NAMNA MATUMIZI YASIYOWAJIBIKA YA MITANDAO YANAVYOTISHIA AMANI YA TANZANIA

JANGA LA KIDIJITI:NAMNA MATUMIZI YASIYOWAJIBIKA YA MITANDAO YANAVYOTISHIA AMANI YA TANZANIA

 

Na Mwandishi Maalumu

Mitandao ya kijamii imefungua milango mikubwa kwa mawasiliano na uhuru wa kujieleza duniani kote, lakini hivi sasa Tanzania inakabiliwa na hatari halisi ya kupoteza udhibiti wa namna nguvu kazi yake kubwa, ambayo ni vijana, inavyotumia majukwaa haya.

 Tatizo kubwa hapa halipo kwenye teknolojia yenyewe ya mitandao, bali liko kwenye matumizi yasiyowajibika yanayoweza kulipua amani na utulivu ambao nchi hii imeilinda kwa miaka mingi sana.

 Hatari hii ya kwanza inachochewa zaidi na kasi ya ajabu ya uenezi wa habari za uongo, ambapo uongo mmoja tu unaopostiwa unaweza kufikia mamilioni ya watu ndani ya dakika chache, na mara nyingi masahihisho huja baada ya uharibifu mkubwa kuwa umeshatokea moyoni mwa jamii.

Katika mazingira ya kisiasa yenye hisia kali, siasa chafu zenye uwakala wa kutumiwa na mataifa ya nje kuhusu masuala ya demokrasia, chaguzi, vurugu, au matamshi ya viongozi wenye tamaa ya madaraka yanaweza kuibua ghasia kabla hata ukweli haujulikana.

 Kimantiki, Watanzania hawapaswi kukubali na lazima wakatae kwa nguvu zote watu wachache wenye nia ovu wanaolipwa fedha nyingi kwa ajili ya kushinda mitandaoni. 

Watu hawa mara nyingi wanaishi kwenye hoteli za kifahari huko Uingereza, Canada, Marekani, Japan na kwingineko, wakichochea vurugu na umwagaji wa damu nchini kwa kutengeneza machapisho bandia yaliyojaa wivu na chuki zao binafsi kwa maslahi ya wale wanaowatuma.

Kibaya zaidi, mitandao hii imegeuka kuwa kiwanda kikubwa cha kuzalisha chuki za kikabila, kidini na kisiasa miongoni mwa wananchi.

 Mifumo ya kidijiti au algoridimu za mitandao hii huwa zinalisha watumiaji yale tu wanayopenda kusikia, hali inayofanya vijana kujifungia kwenye mazingira finyu ambapo upande mwingine wenye mtazamo tofauti unachukiwa badala ya kujadiliwa kwa hoja.

 Unapomzoea mtu unayemwona kuwa adui yako mtandaoni, inakuwa rahisi sana kuamini kuwa ni sawa kumshambulia kwa lugha yoyote ile, jambo linalovunja kabisa mshikamano wa kitaifa ambao umekuwa nguvu na ngao kuu ya nchi tangu kupatikana kwa uhuru.

Hali hii inakwenda sambamba na utamaduni mpya na wa hatari wa kutafuta umaarufu kwa gharama yoyote ile, utamaduni unaosukuma vijana wengi kutumia lugha ya matusi, vitisho, na kejeli ili mradi tu wapate wafuasi na kupendwa mtandaoni.

 Siasa sasa inageuka kuwa burudani ya mapigano ya maneno badala ya kuwa jukwaa la kutafuta ufumbuzi wa changamoto za kijamii. 

Kizazi kinachokua kikiamini kuwa nguvu iko kwenye kupiga kelele zaidi kuliko kujenga hoja zenye mashiko, kitakuwa kizazi cha hovyo kisichoweza kuongoza taifa kwa hekima na busara hapo baadaye.

Kwa bahati mbaya, nchi haina kinga ya kutosha dhidi ya matumizi mabaya yanayoratibiwa kutoka nje ya mipaka yake. 

Udhaifu huu unafanya iwe rahisi kwa watu wasio na nia njema kuingiza propaganda za kigeni, kutengeneza maelfu ya akaunti feki, na kuchezea hisia za vijana ili tu kuvuruga utulivu wa nchi kwa maslahi yao ya kijiografia au kiuchumi. Tanzania ikikaa kimya bila kuchukua hatua dhidi ya uingiliaji huu, inaweza kuamka siku moja na kukuta mgawanyiko mkubwa wa kijamii ambao haukuwahi kutegemewa hapo awali.

Hata hivyo, suluhisho la changamoto hii halianzi kwa serikali pekee bali linaanza na wananchi wenyewe katika ngazi ya mtu mmoja mmoja. 

Kila kijana anapaswa kujiuliza maswali ya msingi kabla ya kubonyeza kitufe cha kusambaza taarifa, akitafakari kama ana ushahidi wa kutosha, kama anaandika kwa ajili ya kujenga au kubomoa, na kama yuko tayari kubeba madhara ya kisheria au kijamii ya maneno yake. 

Ili kufanikisha hili, elimu ya usomaji na uandishi wa kidijiti lazima iingizwe rasmi kwenye mitaala ya shule zetu, huku vyombo vya habari, walimu, na viongozi wa dini wakipaswa kuongoza kwa mfano kwa kutumia lugha safi na hoja zenye msingi.

Tanzania imebaki kuwa visiwa vya amani kwa sababu vizazi vilivyopita vililinda amani hiyo kwa makusudi na kwa gharama kubwa. 

Kwa sababu hiyo, wananchi wa sasa wasidharau kamwe nguvu ya maneno madogo yanayoandikwa kwenye simu zao ndogo za mkononi. 

Ni vyema kukumbuka kuwa chapisho la hasira linalowekwa mtandaoni leo linaweza kuwa chanzo cha kilio na majuto makubwa hapo kesho nchi inapochafuka. Mitandao ya kijamii ni silaha kama silaha nyingine yoyote, na matumizi yake yanahitaji nidhamu ya hali ya juu, hivyo ni wakati sasa wa kuamua kuwa kizazi kinachotumia teknolojia kulinda amani ya nchi na sio kuiharibu.

SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment

Previous Post Next Post