" JUMUIYA YA WAZAZI MPANDA YAFANYA BARAZA LA KIKANUNI, WAJADILI UHAI WA JUMUIYA NA MAENDELEO YA SHULE YA MILALA

JUMUIYA YA WAZAZI MPANDA YAFANYA BARAZA LA KIKANUNI, WAJADILI UHAI WA JUMUIYA NA MAENDELEO YA SHULE YA MILALA

Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Mpanda leo Juni 25, 2026 imefanya Baraza lake la Kikanuni ambapo wajumbe walijadili masuala mbalimbali yanayolenga kuimarisha uhai wa jumuiya, kuongeza wanachama, kuendeleza miradi ya maendeleo pamoja na kufanya maandalizi ya ushiriki katika Maadhimisho ya Wiki ya Wazazi Kitaifa yatakayofanyika Mkoani Mwanza.

Uongozi wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Mpanda ulisisitiza umuhimu wa wanachama wote kuendelea kulipia ada za uanachama ili kuhakikisha jumuiya inaendelea kuwa imara na kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi katika ngazi za matawi, kata na wilaya.

Baraza hilo pia lilijadili mikakati ya kuongeza idadi ya wanachama kupitia kampeni za usajili katika maeneo mbalimbali ya wilaya. Wajumbe walikubaliana kuwa elimu na hamasa ziongezwe ili kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuwahamasisha kujiunga na jumuiya pamoja na kutimiza wajibu wao wa kulipia ada za uanachama.

Ili kurahisisha zoezi hilo, Jumuiya imepanga kutumia maafisa wa TEHAMA kutembelea matawi na kata mbalimbali kwa lengo la kutoa elimu kuhusu namna ya kujiunga na jumuiya na kufanya malipo kupitia simu, mawakala na benki.

Moja ya ajenda kuu zilizojadiliwa katika baraza hilo ni hatma ya Shule ya Sekondari na Ufundi Milala iliyopo Kijiji cha Milala, Kata ya Misunkumilo, ambayo imekuwa haisomeshi kwa kipindi cha miaka mitano.

Wajumbe walieleza kuwa shule hiyo ni mali ya Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Mpanda na ina mchango mkubwa katika maendeleo ya elimu endapo itafufuliwa na kuendelezwa. Kutokana na hali hiyo, baraza lilisisitiza umuhimu wa kupima eneo la shule, kuboresha miundombinu na kuandaa mazingira rafiki yatakayowezesha kuanza tena kwa shughuli za elimu na mafunzo ya ufundi.

Aidha, ilielezwa kuwa shule hiyo bado haina hati miliki ya eneo lake, jambo ambalo limekuwa moja ya changamoto zinazochelewesha maendeleo yake. Viongozi wa jumuiya wameahidi kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha hati miliki inapatikana pamoja na kukamilisha upimaji wa eneo husika.

Baraza lilieleza kuwa shule hiyo inahitaji kiasi cha shilingi milioni 2.3 kwa ajili ya upimaji na upangaji wa eneo, huku likibainisha kuwa taarifa zinazoeleza kuwepo kwa mgogoro kati ya shule hiyo na kanisa si za kweli. Wajumbe walisisitiza kuwa shule hiyo ni mali halali ya Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Mpanda na hakuna mgogoro wowote unaoendelea.

Kutokana na hali hiyo, Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Mpanda imetoa wito kwa wadau wa maendeleo, viongozi na wananchi wenye mapenzi mema kujitokeza kusaidia juhudi za kuifufua shule hiyo ili iweze kutoa huduma za elimu na mafunzo kwa vijana wa Mkoa wa Katavi na maeneo jirani.

Katika hatua nyingine, baraza lilijadili miradi mbalimbali ya kiuchumi inayolenga kuimarisha uwezo wa kifedha wa jumuiya. Wajumbe walihimizwa kubuni na kuanzisha miradi ya kimkakati katika matawi na kata ili kuongeza mapato na kuifanya jumuiya kujitegemea zaidi katika utekelezaji wa shughuli zake.

Baraza hilo pia lilipokea na kujadili taarifa ya tathmini ya Maadhimisho ya Wiki ya Wazazi Wilaya ya Mpanda yaliyofanyika Mei 7, 2026 katika Hospitali ya Halmashauri ya Nsimbo, Kata ya Mtapenda. Wajumbe walitoa pongezi kwa mafanikio ya maadhimisho hayo yaliyohusisha utoaji wa misaada kwa wagonjwa pamoja na upandaji wa miti ya matunda na kivuli.

Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Serikali pamoja na wananchi mbalimbali chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Katavi, Ndugu Evarist Simon Mnyele.

Baraza la Kikanuni la leo pia lilisisitiza umuhimu wa viongozi kuendelea kufanya ziara katika matawi na kata kwa lengo la kutoa elimu kuhusu malezi, mazingira na kuimarisha uhai wa Jumuiya ya Wazazi ndani ya Wilaya ya Mpanda.

Sambamba na hilo, wajumbe walijadili maandalizi ya ushiriki katika Maadhimisho ya Wiki ya Wazazi Kitaifa yatakayofanyika Mkoani Mwanza kuanzia Juni 30 hadi Julai 4, 2026. Baraza lilieleza kuwa ushiriki wa wanachama katika maadhimisho hayo ni muhimu kwa kuimarisha umoja, mshikamano na kubadilishana uzoefu na wanachama kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Mpanda, Ndugu Jimotoli Jilala Maduka, aliwahamasisha viongozi na wanachama kushiriki kikamilifu katika maadhimisho hayo huku akisisitiza kuwa umoja na mshikamano ni msingi wa mafanikio ya jumuiya na Chama Cha Mapinduzi.

Aidha, Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Mpanda ilitumia fursa hiyo kutoa shukrani kwa Waheshimiwa Wabunge, Madiwani pamoja na viongozi mbalimbali wa CCM wanaoendelea kushirikiana na kuisaidia jumuiya katika utekelezaji wa shughuli zake za maendeleo.

Baraza hilo lilihitimishwa kwa wito wa kuendelea kuimarisha mshikamano, ushirikiano na kujitolea katika shughuli za maendeleo kwa manufaa ya jamii na taifa kwa ujumla.

Ndugu Pius M. Buzumalle, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Mpanda, akifungua Baraza la Kikanuni la Jumuiya hiyo leo Juni 25, 2026. Katika baraza hilo, amesisitiza umuhimu wa umoja na mshikamano miongoni mwa wanachama na viongozi ili kuendelea kuimarisha na kuendeleza Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Mpanda. Aidha, aliwakaribisha wajumbe kushiriki kikamilifu katika kujadili agenda mbalimbali na kutoa mawazo yatakayochochea maendeleo ya jumuiya hiyo.



 

Post a Comment

Previous Post Next Post