" KAFULILA AHIMIZA UBIA KUGHARAMIA MIRADI YA MAENDELEO

KAFULILA AHIMIZA UBIA KUGHARAMIA MIRADI YA MAENDELEO

 Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC), David Kafulila amesema Tanzania haiwezi kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa kutegemea kodi na mikopo pekee, akisisitiza umuhimu wa kuimarisha ubia kati ya Serikali na sekta binafsi katika kugharamia na kuendesha miradi ya maendeleo.


Akizungumza katika mhadhara wa kisomi uliofanyika Chuo Kikuu Mzumbe, Kafulila alisema ushiriki wa sekta binafsi ni sehemu muhimu ya mkakati wa kujenga uchumi unaolenga kuboresha maisha ya wananchi.

"Kodi na mikopo haitoshi kuujenga uchumi tunaoutaka. Ndiyo maana dunia imeelekeza nguvu katika ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi ili kuharakisha maendeleo," amesema.

Amesema licha ya baadhi ya wananchi kuamini kuwa Tanzania inakusanya kodi nyingi, ukweli ni kwamba uwiano wa mapato ya kodi kwa Pato la Taifa (tax-to-GDP ratio) ni takribani asilimia 13, kiwango ambacho kiko chini ya wastani wa Afrika wa asilimia 16.

Kafulila ameongeza kuwa mafanikio ya ubia hayategemei mtaji wa fedha pekee, bali pia maarifa na uwezo wa kusimamia miradi kwa ufanisi.

"Thamani siyo kuja na mitambo pekee. Maarifa yana thamani kubwa. Unaweza ukakuta Serikali imejenga reli, imenunua mabehewa na miundombinu yote, lakini mwekezaji analeta utaalamu wa kuiendesha kwa faida. Huo nao ni mtaji," alisema.

Aidha amefafanua kuwa sheria ya ubia nchini inaruhusu mifumo mbalimbali ya utekelezaji wa miradi, ikiwemo miradi inayopendekezwa na wawekezaji binafsi (unsolicited proposals), mazungumzo ya moja kwa moja pale kunapokuwa na uhitaji wa dharura, pamoja na utaratibu maalumu (special regime) kwa miradi yenye maslahi ya kimkakati.

Akitoa mfano, amesema mwekezaji anaweza kubaini fursa ya kujenga hosteli ndani ya chuo kikuu na kuwasilisha pendekezo la mradi wa ubia bila kusubiri Serikali kutangaza zabuni.

Katika hotuba yake, Kafulila pia amesisitiza umuhimu wa vyuo vikuu kuzalisha wahitimu wenye uwezo wa kutatua changamoto za maendeleo badala ya kuishia kuwa na vyeti pekee.

"Unaweza ukasoma mpaka PhD, lakini kama siyo productive wewe ni liability. Vivyo hivyo, mtu mwenye elimu ya darasa la saba anaweza kuwa asset kama anazalisha na kuongeza thamani katika uchumi," amesema.

Amesema elimu inapaswa kujengwa katika mfumo unaozingatia umahiri (competency-based education) ili kuzalisha rasilimali watu yenye uwezo wa kubadilisha maliasili kuwa uchumi unaowanufaisha wananchi.

Kafulila amesema falsafa hiyo ndiyo iliyokuwa msingi wa mawazo ya Hayati Mwalimu Julius Nyerere kupitia sera ya Education for Self-Reliance, ambayo ililenga kutumia elimu kama chombo cha kujenga maendeleo ya watu na taifa.

Post a Comment

Previous Post Next Post