
Mwanafunzi wa Kidato cha Nne katika Shule ya Sekondari Bukimau, iliyopo Kata ya Bumilayinga katika Halmashauri ya Mji wa Mafinga, Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa, amefariki dunia kufuatia tukio la kushambuliwa linalodaiwa kutokea akiwa shuleni.
Marehemu ametambulika kwa jina la Kojak Emily Ungele (19), ambaye alifariki dunia usiku wa kuamkia Juni 1, 2026, katika mazingira ambayo kwa sasa yanachunguzwa na vyombo vya dola.
Taarifa za awali zinaeleza kuwa tukio hilo linahusishwa na tuhuma za wizi wa mashine ya kunyolea nywele pamoja na redio, ambapo mwanafunzi huyo alidaiwa kuhusishwa na tukio hilo kabla ya kupata madhara yaliyosababisha kifo chake.
Baada ya tukio hilo, mwanafunzi huyo alipelekwa katika Kituo cha Afya cha Nyororo kwa ajili ya kupatiwa matibabu ya haraka. Hata hivyo, taarifa kutoka kituoni hapo zinaeleza kuwa alipofikishwa alikuwa tayari ameshafariki dunia.
Kufuatia kifo hicho, Jeshi la Polisi limeanza uchunguzi wa kina ili kubaini mazingira halisi ya tukio hilo. Polisi wanawashikilia watu kadhaa kwa mahojiano, akiwemo mwalimu mlezi wa shule hiyo pamoja na wanafunzi wengine wanaodaiwa kuhusika kwa namna mbalimbali katika tukio hilo.
Kifo hicho kimezua simanzi kubwa kwa familia, ndugu, jamaa na wakazi wa Mafinga, huku wengi wakitaka ukweli wa tukio hilo ujulikane na hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya yeyote atakayebainika kuhusika.
Akizungumza nyumbani kwa familia hiyo katika Mtaa wa Kinyanambo A, mjini Mafinga, baba mzazi wa marehemu, Emily Ungele maarufu kama Kaka Pesa, alisema walipokea taarifa kutoka kwa walimu wa shule hiyo zikieleza kuwa mtoto wao alikuwa amepata madhara na amekimbizwa hospitalini kwa matibabu.
Alisema familia iliwahi kufika katika Kituo cha Afya cha Nyororo kwa matumaini ya kumwona mtoto wao akiwa hai, lakini walipofika walipewa taarifa kuwa alikuwa tayari amefariki dunia.
“Tulipewa taarifa kutoka shuleni kwamba mtoto wetu alikuwa amepelekwa hospitali kwa matibabu. Tulipofika tulielezwa kuwa tayari ameshafariki dunia. Ni jambo la kusikitisha sana kwa familia yetu,” alisema baba huyo kwa huzuni.
Wakazi wa eneo hilo wameeleza masikitiko yao kufuatia tukio hilo na kuitaka mamlaka husika kuhakikisha uchunguzi unafanyika kwa haraka na kwa uwazi ili kubaini ukweli wa kilichotokea.
Jeshi la Polisi limeendelea kusisitiza kuwa uchunguzi unaendelea na kwamba hatua stahiki za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaobainika kuhusika na tukio hilo. Wakati huo huo, viongozi wa elimu na jamii wamehimizwa kuimarisha mifumo ya ulinzi na usalama mashuleni ili kuzuia matukio yanayoweza kuhatarisha maisha ya wanafunzi.
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment