" USHIRIKIANO WA JMAT NA SUNGUSUNGU WATAJWA NGUZO YA AMANI SHINYANGA

USHIRIKIANO WA JMAT NA SUNGUSUNGU WATAJWA NGUZO YA AMANI SHINYANGA

Na Mwandishi wetu –Shinyanga
Viongozi wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) Mkoa wa Shinyanga wamekutana na viongozi wa Jeshi la Jadi Sungusungu ngazi ya Manispaa ya Shinyanga katika kikao cha kawaida kilicholenga kuimarisha ushirikiano katika kulinda amani, kuzuia uhalifu na kuendeleza ulinzi shirikishi kwa manufaa ya wananchi.
Akifungua kikao hicho, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Mkoa wa Shinyanga, Sheikh Balilusa Khamis, ametoa wito wa kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Sungusungu, wananchi na vyombo vya ulinzi na usalama katika kubaini mapema mianya ya uhalifu, kutambua viashiria vya vitendo vya kihalifu na kutoa taarifa kuhusu wahalifu.
Amesema ushirikiano huo utaendelea kudumisha amani na utulivu, hali itakayowawezesha wananchi kuishi katika mazingira salama na kujikita kikamilifu katika shughuli za uzalishaji na maendeleo ya kiuchumi.
Kwa upande wake, Kamanda wa Jeshi la Jadi Sungusungu Mkoa wa Shinyanga, John Kadama, amesema jeshi hilo limeendelea kutekeleza jukumu lake la kulinda usalama wa wananchi kwa kushirikiana kwa karibu na Jeshi la Polisi kupitia mfumo wa ulinzi shirikishi, ikiwa ni pamoja na kubaini viashiria vya uhalifu, kuwafichua wahalifu na kutoa taarifa kwa mamlaka husika.
Kadama amesema ushirikiano huo umechangia kuendelea kuimarika kwa hali ya amani na utulivu katika Mkoa wa Shinyanga, huku akimpongeza Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro, pamoja na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Janeth Magomi, kwa ushirikiano wao wa karibu na Jeshi la Jadi Sungusungu.
Amesema viongozi hao wamekuwa daraja muhimu la kuimarisha mahusiano kati ya Sungusungu, Serikali na wadau wengine wa usalama, jambo linalowapa ari na nguvu ya kuendelea kutekeleza wajibu wao kwa ufanisi.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Wazee Manispaa ya Shinyanga, Stephano Tano, amesema Jeshi la Jadi Sungusungu limekuwa na mchango mkubwa katika kudumisha amani kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, huku akitoa wito kwa wadau wote wa amani kuendelea kuunganisha nguvu ili kulinda utulivu uliopo.
Amesema Sungusungu limeendelea kuwa mfano wa uzalendo na uwajibikaji katika masuala ya ulinzi wa jamii, hatua iliyochangia wananchi kuishi katika mazingira salama na yenye amani.
Kwa upande wake, Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Shinyanga, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Fraterine Tesha, amewataka Sungusungu kuendelea kushirikiana kwa karibu na Jeshi la Polisi katika kuimarisha ulinzi shirikishi na kulinda tunu za taifa zilizoasisiwa na waasisi wa Tanzania.
ACP Tesha amesema Jeshi la Polisi limeendelea kuboresha mifumo yake ya kiutendaji na kuongeza weledi pamoja na uadilifu katika utoaji wa huduma, hatua ambazo zimeongeza imani ya wananchi kwa jeshi hilo na kuimarisha ushirikiano katika mapambano dhidi ya uhalifu.
Naye Kiongozi wa Mila na Desturi, Mkoa wa Shinyaga Mtemi Kidola wa Pili, amesema Jeshi la Jadi Sungusungu limeendelea kuaminiwa na jamii kutokana na uwezo wake wa kutumia maarifa ya kimila na mbinu za jadi katika kubaini viashiria vya uhalifu na wahalifu.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa juhudi hizo zinapaswa kuendelea kufanyika kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi na kwa kuzingatia sheria, taratibu na haki za wananchi ili kuendelea kudumisha amani na usalama katika jamii.
Kikao hicho pia kilihudhuriwa na wadau mbalimbali wa amani na usalama, wakiwemo viongozi wa Jeshi la Polisi, Katibu wa mbunge, Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Wazee Manispaa ya Shinyanga, Afisa Mtendaji wa Kata ya Kambarage, pamoja na viongozi wa Jeshi la Jadi Sungusungu ngazi ya Manispaa ya Shinyanga.
Washiriki hao walisisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya jamii, Serikali na vyombo vya ulinzi na usalama katika kudumisha amani, utulivu na usalama wa wananchi.




SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254



 

Post a Comment

Previous Post Next Post