" VIJANA WAJASIRIAMALI ELFU77 WAFUZU MAFUNZO YA MATUMIZI SAHIHI YA FEDHA, WATAKIWA KUSAMBAZA ELIMU HIYO KWA WENGINE

VIJANA WAJASIRIAMALI ELFU77 WAFUZU MAFUNZO YA MATUMIZI SAHIHI YA FEDHA, WATAKIWA KUSAMBAZA ELIMU HIYO KWA WENGINE

Na Seif Mangwangi, Arusha

ZAIDI ya vijana elfu 77, kutoka mikoa nane wanaojishughulisha na ujasiriamali wa kilimo na ufugaji nchini, wamepatiwa mafunzo ya matumizi sahihi ya fedha Ili kuwasaidia kuboresha shughuli zao na jamii inayowazunguka.

Mafunzo hayo ambayo yametolewa na chuo cha Benki Kuu ya Tanzania (BOT), kwa ufadhili wa mfuko wa chakula Duniani (WFP), vijana hao wametoka katika mikoa ya Arusha, Manyara, Morogoro, Dodoma, Shinyanga, Simiyu, Tabora na Singida.
Viongozi wa chuo cha Benki Kuu ya Tanzania pamoja wakiongozwa na Mkuu wa chuo hicho Dkt Nicas Yuna na waratibu wa mafunzo hayo kutoka WFP wakiwa kwenye picha ya pamoja na maafisa maendeleo ya Jamii waliokuwa wakihudhuria mafunzo hayo



Akizungumza wakati wa kufunga mahafali ya kuhitimu mafunzo hayo kwa vijana kutoka mikoa mitano ya Morogoro, Arusha, Singida, Dodoma na Manyara leo Juni25,2026 Mkuu wa chuo cha benki Kuu Tanzania, Dr Nicas Yuna amesema elimu waliyopewa vijana hao ni silaha ya kuwakwamua kiuchumi.

Amesema vijana hao wanatakiwa kutumia elimu waliyoipata kupitia  mafunzo hayo kuwafundisha vijana wengine na kwamba chuo cha benki kuu kitafuatilia kujua matokeo ya mafunzo hayo kwa Kila kijana aliyehudhuria.

“ Haya ni mafunzo ambayo yanatakiwa kusambaa zaidi, na hawa ni vijana wachache walioteuliwa Ili waweze kwenda kuwa walimu Kwa vijana wengine, tunaamini wakiisambaza elimu hii vizuri, vijana wengi watafaidika na kujikwamua kiuchumi,” amesema Dkt Yuna.

Amesema katika mafunzo hayo ambapo pia walialikwa wakufunzi kutoka taasisi za benki ili kutoa elimu ya namna ya kukopa, bima kwaajili ya usalama wa mazao na mifugo pamoja na mfuko wa uwekezaji UTT, walifundishwa masomo ya namna ya kutafuta fedha halali, kubana na kutunza fedha kwaajili ya uwekezaji.

Afisa habari wa WFP nchini, Brigitha Lyimo amesema mafunzo hayo ni muendelezo wa mradi wa miaka mitano wa vijana kilimo Biashara kwaajili ya kuwawezesha vijana katika ujasiriamali wa kilimo ulioanza mwaka 2023.

Kaimu Mkurugenzi wa WFP nchini Tanzania, Christine Mendes amelishukuru shirika la Mastercard foundation Kwa ufadhili wa programu hiyo ya kumwezesha kijana na kusema ni matarajio ya WFP kuwa wahitimu wa mafunzo hayo wataenda kuibadilisha jamii wanayotoka kwa kuendeleza kilimo na ufugaji kwa kutumia mbinu za kisasa za matumizi sahihi ya fedha.


“ Kwa msaada wa mfuko wa wakfu wa Mastercard, WFP inatekeleza programu ya Vijana Kilimo Biashara (VKB), Ili kuunda na kutengeneza fursa za kazi zenye heshima na utiifu Kwa vijana kupitia mnyororo wa thamani ya kilimo,pia programu hii inatambua kuwa uwezo wa kifedha ni muhimu kwa ujasiriamali, ukuaji wa biashara na mabadiliko ya muda mrefu ya kiuchumi,” Amesema.

Amesema katika mahafali hayo ambapo jumla ya wahitimu walimu wa fedha 79 walihitimu na kukabidhiwa vyeti, kunakamilisha idadi ya wahitimu 150 kufuatia vijana wengine71 kuhitimu mafunzo ya aina hiyo hiyo Jijini Mwanza na kwamba Mtandao huo unaokua unawakilisha uwekezaji muhimu Kwa watu na taasisi ambao utaendelea kuimarisha ushirikishwaji wa fedha Tanzania nzima.

Amesema mafunzo hayo yatawasaidia vijana kukuza ujasiri wa kuweka akiba, kuwekeza, kuweka rekodi, kupata huduma za kifedha na kufanya maamizi sahihi ya kibiashara.
Mmoja wa wahitimu wa mafunzo ya ualimu wa fedha ambaye pia ni Afisa maendeleo ya Jamii na mratibu wa Ukimwi Halmashauri ya Meru, Lily Msemo akipokea cheti kutoka Kwa Mkuu wa chuo cha benki kuu Tanzania Dkt Nicas Yuna.

Post a Comment

Previous Post Next Post