" WALALAZE: TRA, TUMEJIPANGA KUFANIKISHA MAKUSANYO YA KODI KWA MAENDELEO

WALALAZE: TRA, TUMEJIPANGA KUFANIKISHA MAKUSANYO YA KODI KWA MAENDELEO

NA: MWANDISHI WETU, DODOMA 

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambayo ni miongoni mwa taasisi chini ya Wizara ya Fedha imejipanga kuhakikisha kuwa bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027 inafanikiwa kikamilifu katika utekelezaji wake.

Hayo yameelezwa na Meneja wa Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Paul Walalaze, Juni 26, 2026, Jijini Dodoma.

Walalaze amesema, bajeti nzima ni shilingi trilioni 62.33, ila TRA ina jukumu kuhakikisha inafanikisha makusanyo ya shilingi trilioni 36.99, ili mipango mizuri iliyowekwa na serikali katika kukuza maendeleo na ustawi wa wananchi ifanikiwe.

"TRA inaendelea kusimamia mkakati wa utiifu wa hiari kupitia utoaji wa elimu kwa walipakodi kwa kutumia vyombo vya habari, mitandao ya kijamii na mlango kwa mlango. Kimsingi, wananchi wakielimishwa ipasavyo juu ya umuhimu wa kulipa kodi na namna kodi hizo zinavyoweza kuleta maendeleo, hawana shida wanalipa, na ndiyo maana TRA tumeimarisha sana elimu ya mlipakodi na matunda yake tumeyaona," amesema Walalaze.

Aidha, Walalaze amesema, mkakati mwingine ambao umeonyesha matokeo chanya na utaendelea kuimarishwa ni kuhimiza mifumo ya kieletroniki ya ukusanyaji mapato na kufuatilia miamala ya malipo.

"Malipo yanapofanyika kieletroniki yanakwenda moja kwa moja panapohusika na kuepusha mianya ya upotevu wake. Hili limehimizwa sana katika bajeti ya mwaka huu, na TRA tunalisimamia hili kikamilifu," amesema.

Katika hatua nyingine, Walalaze amesema, TRA imejipanga kuhakikisha maeneo yote ya forodha yanaimarishwa ili Mamlaka ipate mapato yake ambayo ni chachu ya maendeleo kwa wananchi. Hii ina maana kwamba, TRA itasimamia kikamilifu kazi za forodha kama bandarini na mipakani.

"Maeneo yote ya forodha kama bandarini na mipakani yataimarishwa, na kila bidhaa inayopaswa kulipiwa kodi, italipiwa kwa mujibu wa sheria za kodi. Hii litaijengea uwezo Mamlaka kupata mapato ili kuiwezesha serikali kufanikisha mipango ya maendeleo kwa wananchi," amesisitiza.

Mikakati mingine ambayo TRA imejipanga nayo ni pamoja na kuongeza usajili wa walipakodi wapya hasa wa sekta isiyo rasmi ikiwa ni mpango wa kujumuisha sekta zote yaani sekta rasmi na isiyo rasmi katika ujenzi wa Taifa.

Vilevile, kutumia teknolojia za malipo na mifumo ya kidijitali ili kufuatia biashara ambazo hapo awali hazikuwa kwenye mifumo ya kikodi inayotambulika na serikali.

Mikakati mingine ni kuongeza ushirikiano baina ya TRA na wafanyabiashara bila kusahau utoaji wa elimu mahsusi juu ya mabadiliko ya sheria za fedha ili kujenga uelewa wa pamoja kwa walipakodi na wananchi kwa ujumla.

Halikadhalika, Walalaze amesema, TRA inapoadhimisha miaka 30 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1996, inavijunia mwamko mkubwa walionao wananchi katika kulipa kodi kwa hiari. 

Sambamba na hilo, Mamlaka inajivunia namna serikali inavyotumia vyema kodi zinazokusanywa katika kuboresha huduma za jamii, kukuza maendeleo na ustawi wa wananchi, huku mapato ya ndani yakitegemewa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa asilimia 74.2 katika bajeti ya mwaka 2026/2027, jambo ambalo ni la kihistoria katika nchi yetu.

Kimsingi, TRA imepata mafanikio makubwa katika utendajikazi wake hasa baada ya kufuata maelekezo ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ambaye ameonya matumizi ya mabavu katika ukusanyaji wa kodi huku akihimiza uwepo wa mazungumzo pindi mlipakodi anapokwama kulipa kodi kwa wakati.

SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment

Previous Post Next Post