Mbinga, Ruvuma
Wananchi wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma wanatarajia kunufaika na ujenzi wa barabara ya Utiri–Mahande yenye urefu wa kilomita 14 inayojengwa kwa kiwango cha lami mradi unaotarajiwa kuimarisha usafirishaji wa mazao, kurahisisha huduma za kijamii na kuchochea ukuaji wa uchumi wa eneo hilo.
Mradi huo umefikia asilimia 85.31 ya utekelezaji na unatarajiwa kukamilika mwezi Agosti mwaka huu hali inayowapa matumaini wananchi waliokuwa wakikabiliwa na changamoto za usafiri hususan wakati wa mvua.
Akizungumza wakati wa ziara ya Kamati ya Ukaguzi ya TARURA, kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Bw. Henry Kaywanga amesema lengo la ziara hiyo ni kujionea maendeleo ya mradi huo na kuhakikisha unatekelezwa kwa viwango vinavyokusudiwa ili kutoa manufaa yaliyotarajiwa kwa wananchi.
"Kamati hupokea taarifa za utekelezaji wa miradi mbalimbali lakini pia hutenga muda wa kutembelea maeneo ya kazi ili kujiridhisha na maendeleo yake pamoja na kutoa ushauri utakaosaidia miradi hiyo kukamilika kwa wakati na kutoa huduma bora kwa wananchi", amesema Bw. Kaywanga.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Barabara TARURA, Mhandisi Venant Komba amesema barabara hiyo inajengwa kupitia mradi wa Agri-Connect unaofadhiliwa na Jumuiya ya Ulaya ukiwa na lengo la kuboresha miundombinu inayorahisisha usafirishaji wa mazao ya kilimo kutoka mashambani hadi sokoni hususan kahawa.
Ameeleza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutapunguza gharama na muda wa usafirishaji wa mazao, kuongeza fursa za biashara na kuinua kipato cha wakulima pamoja na wananchi wa Mbinga kwa ujumla.
"Mradi huu utachochea ukuaji wa uchumi wa wananchi kwa kuhakikisha mazao yanasafirishwa kwa urahisi na kwa wakati tofauti na ilivyokuwa hapo awali", amesema Mhandisi Komba.
Naye, mkazi wa Mbinga Bw. Joseph Mbilinyi ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya barabara akisema ujenzi wa barabara hiyo ni ukombozi mkubwa kwa wananchi.
Amesema pamoja na kurahisisha usafiri na usafirishaji wa mazao, barabara hiyo itaongeza upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii na kufungua fursa mpya za maendeleo kwa wakazi wa eneo hilo.
Kamati ya Ukaguzi ya TARURA chini ya kaimu Mwenyekiti wake Bw. Henry Kaywanga inaendelea na ziara za kukagua miradi mbalimbali nchini ili kuhakikisha inatekelezwa kwa ufanisi, ubora unaotakiwa na kuleta matokeo chanya kwa wananchi.
Post a Comment