
Ili kuelewa msukosuko huu, lazima turudi mwanzo.
CHADEMA (Chama cha Demokrasia na Maendeleo) kilianzishwa rasmi mwaka 1992 wakati Tanzania ilipokuwa ikibadili mfumo wa vyama vingi. Waanzilishi wake walikuwa mchanganyiko wa wanasiasa, wanaharakati na watu wa sekta binafsi waliotaka mfumo wa kisiasa unaoweka msisitizo katika uwajibikaji na uhuru wa kiuchumi.
Miongoni mwa watu waliotajwa katika historia ya chama hicho kuna majina ya viongozi kutoka sekta mbalimbali, akiwemo Edwin Mtei, mwanasheria mashuhuri Bob Makani na wengine wengi. Hawa hawakuwa wanamapinduzi; walikuwa mabepari waliochoshwa na uendeshaji wa serikali ya wakati huo.
Wafadhili wa awali: Wafanyabiashara na sekta binafsi
Katika miaka ya mwanzo, CHADEMA kilivutia msaada wa watu wenye uwezo na wafanyabiashara waliotaka sera zinazorahisisha biashara na uwekezaji.
Michango hiyo mara nyingi haikuwekwa hadharani; ilitolewa kwa njia za ndani au kwa msaada wa kimkakati ili kuimarisha miundombinu ya chama na kukijenga mikoani. Kujiunga kwa viongozi wenye umaarufu kuliongeza mvuto wa chama kwa wafadhili na wafuasi.
CHADEMA kilikua kwa kasi kubwa baada ya Edward Lowassa kutangaza kujiunga nacho mwaka 2015, hatua iliyosababisha gumzo kubwa, kuongeza umaarufu wa chama na kuvunja rekodi katika historia ya siasa za vyama vingi nchini.
Kujiunga kwake kulionyesha uwezo wa CHADEMA kuvutia viongozi wa ngazi ya juu kutoka upande mwingine wa kisiasa. Mabepari walifungua mikoba yao, wakimimina fedha nyingi kuunga mkono chama.
Hata hivyo, kila kitu kilibadilika baada ya kuingia kwa uongozi mpya wa Tundu Lissu. Uongozi wake pamoja na wa viongozi wenzake wa kisiasa uliashiria mabadiliko ya mwelekeo wa chama kuelekea masuala ya haki za kiraia, uwazi na masuala ya kijamii. Hii ilileta mabadiliko ya mtazamo wa chama ambayo baadhi ya wafadhili waliona hayakuwa yanalenga kuendeleza maslahi ya kiuchumi.
Athari na changamoto za mabadiliko bila mkakati
Mabadiliko haya ya mwelekeo wa chama yameathiri vyanzo vya ufadhili wa shughuli za CHADEMA katika nyanja kadhaa.
Ni wazi CHADEMA imepoteza uaminifu wa baadhi ya wafadhili kutoka sekta binafsi. Hususan, kundi la wafanyabiashara wanaotaka sera za soko huria limesita kuendelea kutoa michango baada ya chama kuonyesha msimamo wa kisoshalisti au kukosoa sekta binafsi bila kujaribu kuelewa changamoto zao.
Upungufu wa rasilimali za kampeni umeonekana wazi. Bila michango mikubwa, chama kinakosa uwezo wa kuendesha kampeni za kitaifa, kugharamia miundombinu ya chama na kumudu gharama za kisheria pamoja na mahitaji ya wanachama.
Hizi ni baadhi ya athari za mabadiliko yaliyotokana na chama kujikita zaidi kwa wanaharakati wanaoamini kuwa "wafanyabiashara hawana shida." Mabadiliko ya mwelekeo bila mkakati wa kuunganisha makundi tofauti ya wafuasi—wafanyabiashara, wanaharakati na wanasiasa wa jadi—yameacha pengo katika utekelezaji.
CHADEMA sasa inahitaji sera zinazoonyesha jinsi masuala ya kijamii, kama kupunguza umaskini, yanavyoweza kuendana na sera za kukuza biashara ili kuwashirikisha wafadhili na wafuasi kwa pamoja.
Wafanyabiashara na wawekezaji wanaoutazama uongozi huu wanaona chama kinachobeza matatizo yao na kuwafanya kuwa maadui. Kwa nini mfanyabiashara awekeze katika chama kinachomtukana?
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment