" MEJA JENERALI MSTAAFU MUHUGA MFANO WA KUIGWA

MEJA JENERALI MSTAAFU MUHUGA MFANO WA KUIGWA

 

Ofisa Oparesheni wa miradi wa Kampuni ya RM Holding Limited, Carlos, Muhuga akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani), katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam Sabasaba yaliyofikia tamati Julai 13, 2026.

............................ 

Na Claudia Kayombo

BAADA ya kulitumikia Jeshi la Ulinzi la Wananchi Watanzania (JWTZ), katika nyadhifa mbalimbali, ingekuwa sababu kwake ya kutojishughulisha na jambo jingine la kujiingizia kipato.

Huenda angeweza kuwaza ajifanyie kazi rahisi na muda mwingi akitumia kupumzika, kula na kunywa vinywaji laini kuupa burudani mwili wake.

Lakini imekuwa tofauti kwa Meja Jenerali mstaafu, Raphael Muhuga. Yeye aliwaza ajikite katika kilimo bora cha kisasa ufugaji wa ng’ombe, samaki, mbuzi na kondoo pamoja na  kuku wa kisasa.

Kwake hakuona kama kukumbatia pensheni ni jambo la msingi badala yake akaona bora atumie nguvu na maarifa aliyojaliwa na Mungu, kuanzisha kilimo na ufugaji ili kujiongezea kipato na kutoa fursa ya ajira kwa wengine wanaomzunguka.

Uzalishaji huo wenye tija anaufanya chini ya mwamvuli wa Kampuni aliyoifungua ya RM Holding Limited, sanjari na kiwanda cha kisasa cha kuzalisha mchele chenye mashine yenye uwezo wa kugawa madaraja manne ya mchele, daraja la kwanza ndilo bora zaidi, daraja la pili, tatu na la nne ambalo ni la mwisho.

Kwenye Maonesho ya Biashara ya Kimataifa maarufu kama Sabasaba ambako bidhaa zake zilibamba vilivyo, Ofisa oparesheni wa miradi wa kampuni hiyo , Carlos Muhuga, anasema kilimo hicho cha mpunga, baba yake Meja Jenerali mstaafu Muhuga anakifanya Chita mkoani Morogoro huku kiwanda hicho cha kuchakata mpunga na kuongeza thamani kwa maana mchele, kikijengwa Ifakara eneo la Katindiyuka, mkoani humo.

Anasema kiwanda hicho ni kikubwa katika Bonde la Kilombero kina uwezo wa kuchakata mpunga tani sita kwa saa moja na kuwa kina stoo yenye uwezo wa kuhifadhi magunia ya mpunga 150. 

Anasema ufugaji wa ng’ombe, mbuzi. Kondoo na kuku unafanyika  Kirasarawe II eneo la Vumilia Ukooni, mkoani Dar es Salaam huku mabwawa makubwa sita ya ufugaji wa samaki yakiwa mkoani Mwanza.

Ofisa oparesheni huyo anasema kupitia kilimo na ufugaji, wametoa ajira za muda na za kudumu kwa watu zaidi ya 50 ambao wengi wao ni wanawake.

Mstaafu huyo ambaye kampuni yake imeshiriki katika Maonesho ya Sabasaba ya mwaka huu ambayo yanatimiza miaka 50 tangu kuasisiwa kwake mwaka 1976, naye ameungana na wajasiriamali mbalimbali nchini na nje ya nchi kuonesha bidhaa zake bora anazozalisha ukiwamo mchele.

Carlos anasema mchele huo soko lake kwa kiasi kikubwa lipo nchini na kwa kiwango kidogo unauzwa nje katika mataifa jirani ikiwamo Rwanda.

Hata hivyo, Carlos akizungumza katika maonesho hayo yaliyoanza rasmi Juni 28, mwaka huu, na kufikia tamati Julai 13, anasema kutokana na kiwanda chao kuwa na mahitaji makubwa ya malighafi kwa maana ya mpunga, wanalazimika pia kununua kutoka kwa wakulima wadogo wanaowazunguka.

Anatanabahisha kuwa Meja Jenerali Muhuga anazo eka 250 hadi 350 na kuwa licha ya kuwa na eneo kubwa mtaji ni mdogo na kueleza kuwa mapato wanayopata bado hayakidhi mahitaji makubwa ya malighafi hiyo katika kiwanda hicho.

Anasema soko la mchele kwa kiasi kikubwa linapatikana hapa nchini licha ya kuwa wakati mwingine unauzwa kwa kiasi kidogo nje ya nchi huku kuku na mifugo mingine nayo soko lake likipatikana hapa nchini.

“Wanunuzi wanakuja shambani kufuata kuku, kwa ujumla hakuna shida kubwa ya soko la mazao ya kilimo na hata mifugo”, anasema.

Anasema licha ya upatikanaji wa soko lakini bado bei ya mchele wakati mwingine inakuwa ni ya chini kutokana na mchele unaotoka nje ya nchi kuuzwa nchini kwa bei nafuu.

Pia anabainisha kuwa gharama ya vipuri na mashine mbalimbali za kilimo ni aghari sana ambapo kuna wakati inakuwa mzigo kwa mjasiriamali kuweza kuzimudu gharama hizo. Aidha, kutokana na bei za mchele kutokuwa linganifu kuna wakati mkulima anapata hasara.

Kuhusu mikopo ambayo inaweza kumkwamua mkulima Carlos anasema siyo rafiki kwasababu haina riba nafuu ukilinganisha na uwekezaji unafanywa katika kilimo.

Anasema Serikali ina nia njema na kazi zinazofanywa na wajasiriamali hapa nchini kinachokwamisha ni watendaji wachache wasiosimamia haki katika nafasi zao.

Anasema bidhaa zao zote mchele, maziwa, mayai nyama za kuku pamoja na samaki zinauzwa katika Supermarket yao iliyopo makao makuu eneo la Mbagala Tuangoma. 

Muonekano wa Kiwanda cha Kuchakata MMpunga cha kampuni hiyo kilichopo Ifakara mkoani Morogoro.
Muonekano wa ghara la kuhifadhia mpunga la kiwanda hicho.
 

Post a Comment

Previous Post Next Post