Na, Egidia Vedasto, Misalaba Media, Arusha.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari amewataka Mawakili wa serikali kufanya kazi kwa kasi inayostahi
li, akisisitiza kuwa kila mmoja anatakiwa kutambua nafasi yake kama daraja la kufanikisha maendeleo na utekelezaji wa Dira ya Taifa.
Amezungumza hayo wakati akifungua mafunzo Jijini Arusha, na kusisitiza kuwa sheria za nchi zinapaswa kuwa chombo cha kuwezesha mafanikio ya maendeleo,na usimamizi wa mikataba ili kulinda maslahi ya Taifa.
Aidha Johari amesema, mafunzo yanayotolewa kwa Mawakili yana umuhimu mkubwa kwa kuwa yanawajengea uwezo wa kusimamia sheria na mikataba yenye tija, ambayo ni msingi wa utawala bora na uchumi imara.
Mwanasheria Mkuu pia amesisitiza matumizi ya teknolojia katika utendaji wa kazi za kisheria ili kuongeza ufanisi, kasi ya utoaji huduma na kukabiliana na changamoto zinazoibuka katika mazingira ya sasa.
Vilevile, amesisitiza umuhimu wa kuheshimu uhuru wa habari na maoni, huku akitaka maamuzi na utekelezaji wa sheria kuendelea kuzingatia na kulinda maslahi mapana ya nchi.
Akihitimisha, amewataka mawakili zaidi ya 600 waliohudhuria mafunzo hayo kuwa watulivu na makini katika kufuatilia mada mbalimbali zitakazowasilishwa ili kuongeza maarifa na kuboresha utendaji wao wa kazi.
Awali akizungumza katika mafunzo hayo Wakili Neema Ringo amesema mafunzo hayo ya siku tatu yatawawezesha kukumbushana, kubadilishana ujuzi hususan katika kipindi hiki cha mabadiliko ya teknolojia.




Post a Comment