Happy Lazaro,Arumeru.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Ndugu Wazo Michael Mwang’onda, ameweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa Jengo la Biashara la Typha Mall lililopo Leganga, Wilaya ya Arumeru, mradi wenye thamani ya Shilingi Bilioni 3 unaotarajiwa kuongeza ajira, kuimarisha biashara na kuchochea ukuaji wa uchumi katika eneo hilo.

Akitoa taarifa ya mradi huo kwa Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa 2026,Mkurugenzi wa Typha Mall -Leganga ,Absalom Pallagyo amesema kuwa mradi huo ulianza mwaka 2019 ukiwa na lengo la kujenga kituo cha kisasa cha biashara kitakachohudumia wakazi wa Leganga, Usa River na maeneo ya jirani, pamoja na wasafiri wanaotumia Barabara Kuu ya Arusha–Moshi.

Aidha kwa sasa ujenzi umefikia hatua za mwisho za ukamilishaji na unatarajiwa kuanza kutoa huduma katika kipindi kifupi kijacho.

Typha Mall itakuwa na maduka ya biashara, supermarket ya kisasa, ofisi za taasisi za umma na binafsi, benki, kampuni mbalimbali pamoja na maegesho ya magari yenye nafasi ya kutosha, hatua inayotarajiwa kuboresha huduma za biashara na kuvutia wawekezaji zaidi katika Wilaya ya Arumeru.

Mradi huo unatarajiwa kuzalisha ajira za muda zipatazo 75 na ajira za kudumu 20, sambamba na kuongeza mapato ya Halmashauri na Serikali kupitia kodi, ushuru na tozo mbalimbali.

” Vilevile unatarajiwa kuifanya Leganga kuwa kitovu kipya cha biashara na uwekezaji huku ukiboresha mandhari ya eneo hilo.”

Akizungumza wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi, ilielezwa kuwa mradi huo ni sehemu ya mchango wa sekta binafsi katika kuunga mkono jitihada za Serikali za kukuza uchumi na kuboresha maisha ya wananchi kupitia uwekezaji wa miradi ya maendeleo.

Viongozi wa mradi pia walitoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuweka mazingira rafiki yanayowezesha uwekezaji na utekelezaji wa miradi yenye manufaa kwa maendeleo ya wananchi.