
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MWENGE wa uhuru umetembelea, kukagua, kuzindua na kuweka jiwe la msingi katika miradi saba ya maendeleo Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara yenye thamani ya shilingi bilioni 57.2.
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro mwalimu Fakii Raphael Lulandala ameeleza hayo wakati akimkabidhi mwenge wa uhuru mkuu wa wilaya ya Kiteto Remidius Mwema katika makabidhiano yaliyofanyika kwenye kijiji cha Ndedo
DC Lulandala ametaja miradi hiyo iliyotembelewa na mwenge wa uhuru uliokimbizwa kilomita 238 kuwa ni mradi wa madawati katika shule ya sekondari Tanzanite na mradi wa maji mji mdogo wa Mirerani.
Ametaja mradi mwingine ni kuweka jiwe la msingi wodi ya wanawake na watoto katika kituo cha afya Mirerani uliojengwa na kampuni ya Chusa mining LTD inayochimba madini ya Tanzanite.
“Pia mwenge wa uhuru umezindua kiwanda cha madini ya kinywe cha kampuni ya Permanent minerals katika kijiji cha Kandasikira kata ya Shambarai,” amesema DC Lulandala.
Ameeleza kwamba wilaya ya Simanjiro imeendelea kuimarisha juhudi za kukabiliana na upungufu wa kinga mwilini (Ukimwi) na malaria na kuhamasisha uchangiaji wa damu salama.
Amesema watu 181 wamejitokeza kupima maambukizi ya VVU wakiwemo wanaume 117 na wanawake 64, kati ya waliopimwa, hakuna mwanaume aliyebainika kuwa na maambukizi mapya, huku mwanamke mmoja akikutwa na maambukizi na kuunganishwa na huduma za matibabu na ushauri.
“Watu waliitikia vyema wito wa kuchangia damu salama, ambapo jumla ya chupa 13 za damu zilikusanywa, zikivuka lengo la chupa 10 lililokuwa limewekwa kwa shughuli hiyo wakati wa mkesha wa mwenge,” amesema DC Lulandala.
Ameeleza kuwa mafanikio hayo yanaonyesha mwamko mkubwa wa jamii kushiriki shughuli za afya na kuunga mkono jitihada za serikali za kuzuia maambukizi ya VVU, kupambana na malaria na kuhakikisha upatikanaji wa damu salama kwa ajili ya kuokoa maisha ya wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo.
Hata hivyo, kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa mwaka 2026, Wazo Mwang’onda ameipongeza halmashauri ya wilaya ya Simanjiro kwa kuutendea haki mwenge wa uhuru.
“Nawapongeza viongozi na wananchi wa Simanjiro kwa kujitokeza kwa wingi kuulaki mwenge wa uhuru, hamasa kubwa pia miradi bora ya maendeleo iliyopitiwa,” amesema Mwang’onda.
Mwenge wa uhuru umeendelea na mbio zake Wilaya ya Kiteto baada ya kumaliza mbio zake kwa mafanikio makubwa Wilaya ya Simanjiro, kisha halmashauri za Wilaya ya Babati, Mji wa Babati, Wilaya ya Mbulu, Mji wa Mbulu na Hanang’ kabla ya kukabidhiwa Mkoani Singida Julai 18,2026.
Post a Comment