" RAIS SAMIA: WANAHARAKATI WENGINE NI MAGAIDI, ATAJA VITENDO VINAVYOHATARISHA AMANI YA TAIFA

RAIS SAMIA: WANAHARAKATI WENGINE NI MAGAIDI, ATAJA VITENDO VINAVYOHATARISHA AMANI YA TAIFA

 

Na mwandishi wetu,Zanzibar

Rais Samia Suluhu Hassan ametoa onyo kali kwa baadhi ya watu wanaojiita wanaharakati, akisema wapo wanaotumia mwamvuli wa utetezi wa haki za binadamu kujitafutia umaarufu wa kimataifa, ilhali matendo yao yana sifa za ugaidi kutokana na kuhusisha uvunjifu wa amani, uharibifu wa mali na miundombinu ya umma.

Rais Samia amesema ugaidi hauishii kwenye matumizi ya silaha pekee, bali unajumuisha vitendo vinavyolenga kuitishia jamii au kuishurutisha Serikali kukubaliana na matakwa ya mtu au kundi fulani kwa maslahi ya kisiasa, kiitikadi au kidini.

Kauli hiyo ameitoa leo Alhamisi, Julai 9, 2026, visiwani Zanzibar wakati akihutubia katika hafla ya utiaji saini wa Tamko la Pamoja la Maridhiano ya Kisiasa Zanzibar.

Amesema katika mazingira ya dunia ya sasa, kuna makundi yanayotumia mbinu mbalimbali kujaribu kuzuia maendeleo ya nchi zinazopiga hatua kwa kasi, huku yakijificha nyuma ya ajenda zinazojionyesha kuwa za kizalendo.


“Watu au kundi hilo linakuwa na kauli zinazovaa sura ya kizalendo lakini kwa undani ni maslahi binafsi. Mtu anayependa nchi yake kiukweli huijenga na siyo kuibomoa,” amesema Rais Samia.

Aidha, Rais Samia amesisitiza kuwa vitendo vya kigaidi havikubaliki katika nchi yoyote duniani na kwamba mataifa yote hutumia mamlaka ya dola kulinda usalama wa wananchi wake pamoja na heshima ya taifa.

Ameeleza kuwa Tanzania itaendelea kuchukua hatua zote zinazostahili kuhakikisha amani, utulivu na usalama vinaendelea kudumishwa bila kuyumbishwa na watu au makundi yenye nia ya kuvuruga mshikamano wa taifa.

Kauli ya Rais Samia imekuja sambamba na msisitizo wake kuhusu umuhimu wa maridhiano ya kisiasa, akieleza kuwa tofauti za kisiasa zinapaswa kutatuliwa kwa njia ya mazungumzo na kuheshimiana, badala ya vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani na maendeleo ya nchi.

Post a Comment

Previous Post Next Post