" WAZIRI SANGU AHAMASISHA WAJASIRIAMALI KUJISAJILI KUSHIRIKI MAONESHO NCHINI RWANDA

WAZIRI SANGU AHAMASISHA WAJASIRIAMALI KUJISAJILI KUSHIRIKI MAONESHO NCHINI RWANDA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Mhe. Deus C. Sangu, akizungumza na waandishi wa habari mjini Sumbawanga, Mkoa wa Rukwa, leo Julai 23, 2026,kuhusu Tanzania kushiriki katika maonesho ya Wajasiliamali Wadogo (Juakali) ya Afrika Mashariki yatakayofanyika Kigali Rwanda mwezi Oktoba mwaka huu. 

Na: Mwandishi Wetu, SUMBAWANGA

Serikali imetangaza kuwa Tanzania itashiriki Maonesho ya 26 ya Wajasiriamali Wadogowadogo, Wadogo na wa Kati (MSMEs) ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, maarufu kama Nguvu Kazi/Jua Kali, yatakayofanyika jijini Kigali, Rwanda kuanzia Oktoba 30 hadi Novemba 8, 2026.

Akitoa taarifa kwa umma, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Deus Sangu, amesema Tanzania itawakilishwa na wajasiriamali 250 kati ya washiriki wapatao 1,000 wanaotarajiwa kutoka nchi nane wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Amesema kaulimbiu ya maonesho ya mwaka huu ni "Kuendeleza Mnyororo wa Thamani kwenye Sekta ya Ngozi na Kilimo cha Bustani (Matunda na Mbogamboga) katika Ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki."

 "Maonesho hayo yanalenga kuwawezesha wajasiriamali kurasimisha shughuli zao za biashara, kutangaza bidhaa na huduma, kubadilishana uzoefu, kuongeza ujuzi wa uzalishaji pamoja na kupanua masoko ya bidhaa na teknolojia za uzalishaji."amesema Waziri Sangu 

Ameongeza kuwa ushiriki wa Tanzania katika maonesho hayo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuimarisha sekta ya ujasiriamali, kukuza biashara za ndani na nje ya nchi, pamoja na kuongeza fursa za ajira zenye staha kwa Watanzania.

Aidha, Waziri Sangu amewataka wajasiriamali wenye sifa kutumia fursa hiyo kwa kujisajili kushiriki maonesho hayo kuanzia sasa hadi Septemba 30, 2026 kupitia mfumo rasmi wa usajili uliotengwa kwa ajili ya washiriki.

Maonesho ya Nguvu Kazi/Jua Kali ni miongoni mwa majukwaa makubwa ya biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki yanayowakutanisha wajasiriamali, wawekezaji na wadau wa maendeleo kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kuongeza ushindani wa bidhaa zinazozalishwa ndani ya ukanda huo.

Post a Comment

Previous Post Next Post