" FAMILIA YATAJWA KUWA SHULE YA KWANZA YA MAADILI NA MSINGI WA KUZUIA MMOMONYOKO WA KIJAMII

FAMILIA YATAJWA KUWA SHULE YA KWANZA YA MAADILI NA MSINGI WA KUZUIA MMOMONYOKO WA KIJAMII






Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, amesema kuwa familia ndiyo shule ya kwanza ya maadili na inapaswa kuwa msingi imara wa kuwajenga watoto na vijana katika misingi ya heshima, nidhamu, uadilifu, uzalendo na uwajibikaji ili kukabiliana na mmomonyoko wa maadili.


Aidha alisema kwamba kwa sasa mmomonyoko wa maadili unachochewa na kasi ya utandawazi na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii.


Akihitimisha Tamasha la Utamaduni Kitaifa mkoani Morogoro, Msigwa alieleza kuwa mabadiliko ya kiteknolojia yameleta changamoto kubwa katika malezi, ambapo baadhi ya vijana wamekuwa wakikosa nidhamu na kutumia mitandao kusambaza maudhui yasiyofaa na taarifa za uongo, kama ilivyotokea kwake hivi karibuni alipopokea simu za rambirambi kuhusu uzushi wa kifo cha mama yake mzazi ambaye yuko hai na anaendelea na shughuli zake.


Kufuatia hali hiyo, amewasihi Watanzania kurejesha malezi ya nyumbani yanayojikita katika kufundisha watoto bidii, huruma na kuheshimu utu wa wengine, huku akiwakumbusha kutowabeza machifu bali kuwatumia kama rasilimali ya kupata ushauri, uzoefu na miongozo ya kulinda utamaduni wa taifa.


Alisisitiza kuwa mtazamo kuhusu utamaduni unapaswa kubadilika kutoka kuuchukulia kama burudani pekee na badala yake kuutazama kama utambulisho, ajira, biashara na nguvu ya kiuchumi inayojumuisha fursa mbalimbali kama vile muziki, filamu, sanaa za maonesho, mavazi, vyakula vya asili na kazi za mikono.


Aidha, akizungumzia lugha ya Kiswahili, alieleza kuwa ni sehemu muhimu ya utambulisho wa Tanzania na daraja linalounganisha nchi na bara la Afrika pamoja na dunia nzima, jambo linalotaka iendelezwe kikamilifu katika nyanja za elimu, sanaa, utafiti, teknolojia, biashara, utalii na diplomasia ili kukuza uchumi na kulinda heshima ya taifa.

Post a Comment

Previous Post Next Post