" KAIRUKI ATAKA TTCL ILIPE FAIBA KWA GHARAMA INAYOMUDU MWANANCHI

KAIRUKI ATAKA TTCL ILIPE FAIBA KWA GHARAMA INAYOMUDU MWANANCHI



Na Mwandishi Wetu - DAR ES SALAAM


Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki, ameitaka TTCL kuhakikisha huduma ya Faiba Mlangoni Kwako inapatikana kwa gharama nafuu ili familia, wanafunzi, vijana na wafanyabiashara wadogo na wa kati waweze kumudu.

Mhe. Kairuki ametoa kauli hiyo leo Agosti 21,2026, wakati akizindua Awamu ya Pili ya Mradi wa Faiba Mlangoni Kwako katika Ukumbi wa Johari Rotana jijini Dar es Salaam.

Amesema upanuzi wa mtandao wa faiba unapaswa kwenda sambamba na uwepo wa vifurushi vinavyokidhi uwezo wa makundi mbalimbali ya wananchi.

Kwa mujibu wa Waziri, mafanikio ya mradi hayawezi kuishia kwenye ujenzi wa miundombinu, bali yanapaswa kuonekana katika idadi ya wananchi wanaotumia huduma, ubora wa intaneti, kasi na kuridhika kwa wateja.

Ametaka TTCL kuhakikisha huduma inafika katika maeneo yenye makazi yanayokua, masoko, maeneo ya biashara, viwanda, shule, vyuo, vituo vya afya na ofisi za Serikali.

Waziri Kairuki amesema Faiba Mlangoni Kwako ni nyenzo ya kufungua fursa za elimu, biashara, ajira na ubunifu, na kuchochea ujenzi wa uchumi wa kidijitali.


Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, CPA Moremi Marwa, amesema kampuni hiyo inalenga kuongeza zaidi ya Home Pass 400,000 katika Awamu ya Pili, baada ya kujenga zaidi ya 280,000 katika Awamu ya Kwanza.


Marwa amesema TTCL imeendelea kutumia teknolojia ya GPON, ambayo inawezesha kuhudumia wateja wengi, kuongeza ufanisi wa miundombinu na kuboresha ubora wa huduma.


Amesema mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano na makandarasi wa ndani na wa kimataifa, wakiwemo Huawei, ZTT na Visoll.








SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment

Previous Post Next Post