
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka Watanzania kulinda amani na utulivu, akisisitiza kuwa ndiyo msingi wa uwekezaji, ajira na ukuaji wa uchumi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu,Bakari S. Machumu, Rais Dkt. Samia ametoa wito huo leo Ikulu, jijini Dar es Salaam, katika Mkutano Maalum wa Serikali na Sekta Binafsi kuhusu Utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Ameeleza kuwa rasilimali na mitaji mikubwa haziwezi kuleta maendeleo bila mazingira ya amani yanayowapa wawekezaji uhakika na kuwawezesha wafanyabiashara kuendesha shughuli zao bila hofu.
“Katika safari ya Dira 2050, ni wajibu wetu kuilinda amani ya nchi yetu. Tukilinda amani na utulivu, tutakuwa tumelinda uwekezaji, ajira, biashara na kasi ya ukuaji wa uchumi,” amesisitiza.
Rais Dkt. Samia ameitaka sekta binafsi kushiriki katika utekelezaji wa Dira 2050 kwa kuongeza uwekezaji, uzalishaji, huduma, teknolojia na ubunifu, na kuongeza kuwa Serikali itaendelea kuimarisha mazingira ya kisheria, kisera na kitaasisi ili kuvutia uwekezaji wa ndani na nje na kuharakisha utekelezaji wa Dira.
Amehimiza uwekezaji unaounganisha uzalishaji mkubwa na mdogo, biashara kubwa na ndogo, pamoja na matumizi ya ujuzi na wazabuni wa ndani, akihimiza ushirikishwaji wa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu katika uzalishaji na mnyororo wa thamani wa sekta binafsi.
Rais Dkt. Samia ametoa rai kwa wafanyabiashara wa Tanzania na sekta binafsi kuongeza uzalishaji katika sekta za kilimo na viwanda, kuongeza thamani ya rasilimali, kuzingatia viwango vya ubora, sambamba na kupanua shughuli zao nje ya nchi na kuchangamkia masoko ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, Afrika na dunia.
Katika mkutano huo, Rais Dkt. Samia amezindua nyenzo za utekelezaji wa Dira 2050 na kukabidhi Ufunguo wa Mtazamo Mpya, unaoashiria mwanzo mpya wa ushirikiano wenye uwazi na uaminifu kati ya Serikali na sekta binafsi.
Ameitaka Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji kuhakikisha elimu kuhusu nyenzo hizo inawafikia wadau wote muhimu, ili waelewe wajibu wao katika utekelezaji wa Dira 2050.
Kwa upande wake, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameahidi ushirikiano kamili wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika utekelezaji wa Dira 2050.
Ametaja uwekezaji, sayansi, teknolojia, uchumi wa kidijitali, uchumi wa buluu na maendeleo ya rasilimali watu kuwa maeneo muhimu ya ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo, amesema mageuzi ya mazingira ya biashara yameimarisha imani ya wawekezaji na nafasi ya Tanzania katika kuvutia mitaji.
Ametaja kuimarika kwa uwekezaji katika kampuni changa za teknolojia kwenye sekta za fedha, kilimo na nishati safi kuwa ushahidi wa maboresho hayo kuanza kuzaa matunda.
Rais wa Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania, Angelina Ngalula, amepongeza maboresho ya sera, sheria, mifumo ya utawala, uwekezaji na kodi kwa kupanua nafasi ya sekta binafsi katika uchumi.

Wakizungumza kwa niaba ya vyama wanavyoviwakilisha, wawakilishi wa sekta binafsi wameahidi kushirikiana na Serikali kuongeza uwekezaji, teknolojia na ajira, huku wakiiomba Serikali kuendelea kutunga sera zinazotabirika, na kufanya mashauriano endelevu na sekta binafsi kuhusu mazingira ya biashara na uwekezaji.
Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia ameshuhudia utiaji saini wa Tamko la Pamoja kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi kuhusu utekelezaji wa Dira 2050, na kutoa wito kwa taasisi na vyama vilivyosaini Tamko hilo kuwaelimisha wanachama wao, kuliheshimu na kulitekeleza kwa vitendo.
Vilevile, ametunukiwa Tuzo ya Heshima na Sekta Binafsi Tanzania kwa kutambua jitihada zake katika kuboresha mazingira ya biashara, uwekezaji na kukuza uchumi jumuishi nchini.
Rais Dkt. Samia amehitimisha kwa kuzitaka Serikali na sekta binafsi kuendeleza ushirikiano wa kuaminiana, kuongeza kasi ya utekelezaji na kuhakikisha Dira 2050 inaleta matokeo yanayoonekana kwa wananchi.
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254




.jpeg)
Post a Comment