Uzalishaji wa nafaka nchini umeongezeka kutoka tani milioni 11.4 mwaka 2023 hadi kufikia rekodi ya tani milioni 13.9 mwaka 2024, ikiwa ni ongezeko la asilimia 22 ndani ya mwaka mmoja. Takwimu hizo zilitolewa mwaka 2025 na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) kupitia mfumo wa kimataifa wa taarifa na tahadhari ya mapema kuhusu chakula na kilimo, huku mafanikio hayo yakitokana na sera bora, pembejeo, huduma za ugani na juhudi za wananchi.Akifunga Maonesho ya Kilimo, Mifugo, Uvuvi na Sherehe za Nanenane Kitaifa na Kimataifa 2026 katika Viwanja vya John Malecela, Dodoma, Rais Samia Suluhu Hassan aliainisha namna kipindi cha uongozi wake kilivyoweka rekodi mpya katika kuinua sekta ya kilimo, ikiwemo kuongeza bajeti, mikopo, pembejeo na huduma za ugani, huku akitoa maagizo ya kuongeza kasi ya mageuzi hayo.
Alisema Serikali imeongeza bajeti ya Wizara ya Kilimo kutoka Sh bilioni 294 mwaka 2021/22 hadi Sh trilioni 1.105 mwaka 2025/26, na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kutoka Sh bilioni 169.2 hadi Sh bilioni 476.6, sambamba na kuimarisha ruzuku za pembejeo, vyama vya ushirika na ushiriki wa sekta binafsi katika uzalishaji, uhifadhi, masoko na kuongeza thamani ya mazao.
Mtaji wa Benki ya Kilimo Tanzania (TADB) umeongezeka kutoka Sh bilioni 60 mwaka 2021 hadi Sh bilioni 452, huku benki hiyo ikitoa mikopo ya Sh trilioni 1.5 tangu kuanzishwa kwake, ambapo Sh trilioni 1.3 sawa na asilimia 84 zimetolewa chini ya Serikali ya Awamu ya Sita, zikiwemo fedha za mchango wa Sh bilioni 661 kutoka Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), pamoja na Sh bilioni 300 zilizokabidhiwa kwa benki saba kwa ajili ya wakulima, wafugaji na wavuvi.
Katika kuimarisha huduma za ugani, serikali imeanzisha Wakala wa Taifa wa Huduma za Ugani za Kilimo (NAESA) ulioanza kazi Julai mwaka huu na kukabidhiwa magari 48 katika awamu ya kwanza, huku Rais Samia akiagiza shughuli za wakala huo ziingizwe kwenye mifumo ya Serikali za Mitaa, taasisi za utafiti ziongeze ubunifu na teknolojia, na wizara husika zendelee kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji.
Rais Samia pia aliagiza Kanda ya Nanenane ya Nyanda za Juu Kusini igawanywe kutokana na ukubwa wake, akitangaza rasmi kuwa Viwanja vya John Samuel Malecela vitakuwa eneo la kudumu la kilele cha Kitaifa cha Nanenane huku uzinduzi ukizungushwa katika kanda nyingine, na aliwapatia Shilingi milioni 20 vijana wabunifu waliotengeneza ndege nyuki ya kunyunyizia dawa ili kuongeza mtaji na uwezo wa kutengeneza yenye uwezo wa kubeba lita 10 na kuhudumia hekta moja.
Sekta ya mifugo nayo imezidi kuimarika ambapo Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dkt. Bashiru Kakurwa, alieleza kuwa thamani ya mifugo imeongezeka kutoka Sh trilioni 26 mwaka 2020/2021 hadi Sh trilioni 33 mwaka 2024/2025, huku idadi ya ng'ombe ikifikia milioni 40.57, mbuzi milioni 29.99 na kondoo milioni 9.94.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, alieleza kuwa mkoa huo umeimarisha zao la zabibu lenye viwanda 39 vya kuchakata na linaendelea kukuza kilimo cha tufaa kupitia mashamba darasa katika kila wilaya. Maadhimisho hayo yaliyotanguliwa na maonesho kuanzia Agosti 1, 2026, yamebeba kaulimbiu isemayo “Tambua Soko, Ongeza Tija Kutekeleza Dira 2050,” huku Tanzania ikiendelea kutambuliwa kimataifa kwa kushika nafasi nzuri katika utekelezaji wa Azimio la Malabo na mipango ya maendeleo ya kilimo barani Afrika.
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment