Kikundi Kazi cha INTOSAI cha kupambana na Usafirishaji wa Fedha Haramu (WGFACML) Chaketi
Na, Egidia Vedasto,
Misalaba Media, Arusha.
Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichele, amesema wamiliki fiche wa kampuni ni miongoni mwa changamoto zinazoweza kuathiri ushindani katika manunuzi ya umma, ukusanyaji wa kodi na uchumi wa nchi, akizihimiza nchi mbalimbali kuimarisha ushirikiano katika kuwabaini na kuwachukulia hatua.
Akizungumza katika mkutano wa 19 wa INTOSAI Working Group on the Fight Against Corruption and Money Laundering (WGFACML) Jijini Arusha, Kichere amesema mapambano dhidi ya wamiliki fiche si suala la Tanzania pekee, bali ni changamoto ya kimataifa inayohitaji ushirikiano wa nchi mbalimbali katika kubadilishana taarifa na kuchukua hatua.
Amesema ushirikiano huo ni muhimu katika kuhakikisha mifumo ya manunuzi, kodi na biashara inakuwa na ushindani wa haki, inapunguza mianya ya rushwa na utakatishaji fedha, na hatimaye kulinda rasilimali za umma.
"kampuni mbili au zaidi zinaweza kuonekana zikishindana katika zabuni, wakati nyuma yake zikawa zinamilikiwa au kudhibitiwa na mtu mmoja, familia moja au kundi moja la watu wanaojificha nyuma ya majina ya watu wengine",
"Hali hiyo inaweza kuifanya Serikali kuona kuna ushindani wakati kiuhalisia ushindani huo si wa kweli, na unaweza kuisababisha Serikali kununua bidhaa au huduma kwa bei kubwa kuliko thamani yake halisi, kutokana na kampuni zinazohusika kupanga bei kwa namna inayomnufaisha mtu au kundi moja linalozimiliki kwa siri" amesema Kichere.
Pia amebainisha kuwa hali hiyo inaweza kusababisha matumizi yasiyo na tija ya fedha za umma, hasa kwa kuzingatia kwamba sehemu kubwa ya bajeti za Serikali hutumika katika manunuzi ya bidhaa na huduma.
Hatahivyo Kichere, amesema wamiliki fiche wanaweza kuathiri ukusanyaji wa kodi na mapato ya forodha kupitia miamala ya kampuni zinazohusiana, ikiwemo upangaji wa bei za uhamishaji (transfer pricing), hali inayoweza kupunguza mapato ambayo Serikali inapaswa kuyapata. Amesema Tanzania tayari imeweka utaratibu wa kisheria unaozitaka kampuni kutangaza taarifa za umiliki wao, huku matumizi ya mifumo ya kidijitali ya manunuzi, ikiwemo NEST, yakisaidia kuongeza uwazi na kurahisisha ufuatiliaji.
Katika namna hiyohiyo Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Bi.Neema Mwakalyelye, amesema kuimarisha ushirikiano kati ya TAKUKURU na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi ni muhimu katika kudhibiti upotevu wa fedha za umma, hususan katika eneo la manunuzi ya umma na uwazi wa umiliki wa kampuni.
Amefafanua kwamba, uwepo wa sheria imara zinazohusu usajili wa kampuni, uwazi wa wamiliki wa kampuni na udhibiti wa utakatishaji fedha umeongeza uwezo wa taasisi za Serikali kufanya uchunguzi na kuchukua hatua dhidi ya vitendo vya ubadhirifu na rushwa"Sheria hizo zimekuwa nyenzo muhimu katika kuimarisha uwajibikaji na uadilifu katika matumizi ya rasilimali za umma"
"Maboresho yaliyofanyika katika sheria za manunuzi ya umma yamekuwa chachu ya kuimarisha udhibiti wa matumizi ya fedha na mali za Serikali, na yamesaidia TAKUKURU kubaini vihatarishi vya rushwa katika michakato ya manunuzi na utekelezaji wa mikataba ya umma"
Vilevile Bi.Mwakalyelye amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitatu, kuanzia mwaka 2023 hadi sasa, ushirikiano kati ya taasisi hizo umewezesha kufuatilia fedha zinazokadiriwa kufikia Sh bilioni 19.
"Mafanikio hayo yametokana na ushirikiano katika uchunguzi, ukaguzi maalum na uwasilishaji wa ushahidi katika mashauri yanayofikishwa mahakamani. Ushirikiano huo utaendelea kuwa muhimu katika kulinda fedha za Serikali na kuhakikisha fedha zilizopotea zinarejeshwa pale inapobainika kuwa zimepotea" amesema Bi.Mwakalyele.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Manunuzi na Ugavi, Dennis Simba, amesema Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) ni miongoni mwa wadau wanaoshirikiana na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika kuhakikisha rasilimali za umma zinalindwa na kutumika kwa mujibu wa sheria na taratibu.
Simba amesema ushirikiano huo unalenga kuimarisha maeneo muhimu ikiwemo kupambana na rushwa, kufanya uchunguzi na kuhakikisha taratibu za manunuzi ya umma zinafuatwa.
Hata hivyo amesema hatua hizo ni muhimu katika kuongeza uwazi, uwajibikaji na kulinda fedha za Serikali dhidi ya matumizi yasiyo sahihi.
Simba ameeleza kuwa kuanzia mwaka 2020 hadi 2023, mchakato wa ununuzi wa umma umeendelea kufanyika kwa njia ya kidijitali kupitia mfumo wa NEST, hatua ambayo imeongeza ufanisi na uwazi katika mchakato wa manunuzi.
"Mfumo huo pia unasaidia kuweka kumbukumbu za michakato ya manunuzi na kurahisisha ufuatiliaji, eneo lingine muhimu ni utoaji wa taarifa kuhusu wamiliki fiche wa kampuni zinazoshiriki katika zabuni za Serikali, ili kuwezesha mamlaka kubaini iwapo kuna maslahi yaliyofichwa, rushwa au ukiukwaji mwingine wa taratibu. Taarifa hizo ni muhimu katika kuimarisha uadilifu na uwazi katika manunuzi ya umma" amesisitiza Simba
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment