Aliyekuwa mgombea urais kupitia Chama cha Makini, Coster Kibonde alisema uthubutu aliouonesha Rais Samia Suluhu Hassan kutekeleza mradi wa Kituo cha kuzalisha umeme cha Julius Nyerere (JNHPP) kupitia fedha za ndani unadhihirisha serikali imejipanga kuongeza tija kwenye maendeleo ya nchi.
Alisema hayo akizungumzia uzinduzi rasmi wa kituo hicho utakaofanywa na Rais Samia hapo kesho.
“Naipongeza Serikali ya Awamu zote mbili, ya tano na ya sita wameonesha uthubutu mkubwa sana kwa kukamilisha mradi huu, wameionesha dunia kwamba Tanzania tunaweza kujitegema kiuchumi na katika kutafuta maendeleo yetu,” alisema Kibonde.
Aliongeza: “Na hii naomba iwe mfano kwa viongozi na watendaji wengine wa serikali pale wanapoachiwa kijiti na viongozi walioko madarakani wahakikishe wanaitekeleza wasiiache, wasiwe chanzo cha miradi hiyo kuzorota, kukamilishwa kwa viwango vya chini pamoja na kusuasua. Tumeona Rais Samia alichokifanya mradi haukusuasua”.
Kibonde alisema uamuzi wa serikali kutekeleza mradi huo kwa fedha za ndani umeonesha ujasiri kwamba Tanzania ni nchi inayoweza kujitegemea yenyewe. “Kwamba hatuwezi kutegemea fedha za ufadhili ndio tukamilishe miradi yetu na imewezekana, wakati mwingine kutegemea misaada ya masharti ili kufanya maendeleo kwenye nchi madhara yake ni makubwa na yanaumiza wananchi kwa hiyo nashauri serikali iendelee kutekeleza na miradi mingine bila fedha za msaada kwa sababu inawezekana,” alisema.
Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi amesema Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuzindua mradi huo kesho, kikiwa na uwezo wa kuzalisha megawati 2,115 kwa kutumia mashine tisa katika eneo la mradi Rufiji mkoani Pwani.
Ndejembi alisema JNHPP ilianza kujengwa Juni 2019 na kukamilika Machi 2025 na ina uwezo wa kutunza maji ni meta za ujazo bilioni 33 ambazo ni takribani mara 10 ya uwezo wa Bwawa la Mtera.
“Huu ni mradi mkubwa zaidi wa kuzalisha umeme kuwahi kutekelezwa nchini kwa kutumia fedha za ndani za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ukiwa na uwekezaji wa takribani Shilingi trilioni 7.452,” alisema.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia umeme na nishati jadidifu, Felchesmi Mramba amesema ujenzi wa JNHPP umekamilika kwa asilimia 100 na awali gharama ya mradi ilikuwa trilioni 6.5 lakini thamani halisi mpaka unakamilika imefikia trilioni 7.4.
Naye aliyekuwa mgombea urais kupitia Chama cha Wakulima (AAFP), Kunje Ngombale Mwiru alisema kukamilika kwa mradi huo ni ushahidi kwamba kukiwa na dhamira taifa linaweza kutekeleza miradi mikubwa ya kitaifa kwa maslahi ya muda mrefu ya nchi.
Kunje alisema uthubutu wa Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano, Dk John Magufuli na Makamu wake wakati huo, Rais Samia unatuma ujumbe kwamba viongozi wanapaswa kuwa na maono ya muda mrefu na wafanye maamuzi yenye manufaa kwa kizazi cha sasa na kijacho.
“Na hii iwe mfano kwa vyama vya upinzani, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimekuwa na sera bora zinazotekelezeka ndio maana kimeendelea kukaa madarakani kwa muda mrefu, tuige mfano wakati wa kuandaa sera lakini pia tuwe watekelezaji,” alisema.
Kunje alisema katika JNHPP jambo kubwa si tu megawati zinazozalishwa, bali pia uwezo wa serikali kuweka mbele miradi yenye maslahi ya muda mrefu kwa taifa hata kama utekelezaji wake unahitaji rasilimali nyingi. Mradi kama JNHPP unapaswa kuwa somo kwamba miradi mikubwa ya kimkakati inahitaji ujasiri wa kuanza, uvumilivu wa kuendelea na uwajibikaji wa kuhakikisha inakamilika,” alisema.
Alisema wakati serikali ilipotangaza kuanzishwa kwa mradi huo nchi mbalimbali zilionesha kupinga kwa kudai kuwa eneo hilo ni la hifadhi ya wanyama.
“Jambo hili linaonesha umuhimu wa nchi kuwa na uwezo wa kutathmini maamuzi yake kwa kuzingatia mazingira na mahitaji yake yenyewe ndiyo maana Dk Magufuli na Rais Samia hawakutetereshwa na maneno yao, walidhihirisha kwamba hii ni nchi huru na inauweza kujitegemea,” alisema.
Aliyekuwa mgombea urais kupitia Chama Cha Kijamii (CCK), David Mwaijojele alisema uamuzi wa serikali kutumia fedha za ndani umeonesha kiwango cha uwezo wa nchi kujiamulia vipaumbele vyake vya maendeleo.
“Wakati mwingine mikopo na misaada ya nje inakuja na masharti ambayo huongeza mzigo wa madeni. Kwa hiyo pale nchi inapokuwa na uwezo wa kugharamia mradi mkubwa kwa kutumia rasilimali zake inajenga uwezo wa kufanya maamuzi kwa kuzingatia maslahi yake yenyewe,” alisema Mwaijojele.
Alisema uhusiano wa kimataifa ni muhimu kama hauingilii maamuzi ya wengine ndio maana Tanzania haiwezi kutegemea wengine kuamua kila kitu kuhusu maendeleo yake.
“Ndiyo maana viongozi wetu kwa kutambua hilo walisonga mbele na sasa tunafurahia matunda ya misimamo na uthubutu wao,” alisema Mwaijojele.
Mgombea urais kupitia Chama cha Union for Multiparty Democracy (UMD), Mwajuma Mirambo alisema kujitosheleza kwa umeme kuna umuhimu katika uhuru wa kiuchumi na kitaifa. Mirambo alisema umeme wa uhakika ni msingi wa viwanda, biashara, kilimo cha kisasa, huduma za afya, elimu, teknolojia na uwekezaji.
“JNHPP haipaswi kuangaliwa kama mradi wa kuzalisha umeme pekee bali inapaswa kuonekana kama sehemu ya mkakati mpana wa kujenga Tanzania inayoweza kuzalisha, kusindika na kuuza bidhaa zake, badala ya kuwa tegemezi kwa bidhaa na huduma kutoka nje,” alisema.
Mirambo alisema viongozi hawapaswi kuvunjwa moyo na maneno ya nchi nyingine au wanaharakati kwa sababu wamebeba maono ya nchi.
“Wanaharakati na baadhi ya mataifa walipinga uamuzi wa serikali na wengine walisema Tanzania haiwezi sasa viongozi wetu wamepambana na tumeweza, tutakuwa na umeme wa kutosha ambao tutakwenda hata kuwauzia mataifa ambayo yalipinga uamuzi wa serikali,” alisema.
Aliongeza: “Mafanikio ya JNHPP yanapaswa kuwa mwanzo wa hatua nyingine kubwa zaidi za kuifanya Tanzania itumie nishati hiyo”
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment