" Baraza laahidi kuendelea kuishauri serikali masuala ya amani

Baraza laahidi kuendelea kuishauri serikali masuala ya amani




BARAZA la Vyama vya Siasa Tanzania limeahidi kuendelea kuishauri serikali kuhusu mambo yenye manufaa na maslahi mapana kwa taifa, yanayolenga kujenga nchi, kuimarisha amani na kuwaunganisha Watanzania.

Mwenyekiti wa baraza hilo, Juma Ali Khatib alisema hayo wakati wa mkutano wa uchaguzi wa kamati za kisekta za baraza hilo uliofanyika mjini Morogoro juzi.

Katika uchaguzi huo, wenyeviti na makamu wenyeviti waliochaguliwa wataongoza Kamati ya Maadili na Uhusiano, Kamati ya Sheria na Utawala Bora, Kamati ya Masuala ya Uchaguzi na Kamati ya Bunge na Siasa.

Khatib alisema baada ya Uchaguzi Mkuu uliopita, serikali inaendelea na majukumu yake, hivyo jukumu la baraza ni kuwaunganisha wananchi na wanasiasa kwa kuhubiri amani ili wananchi waendelee na shughuli za uzalishaji zitakazowaingizia kipato kwa amani na utulivu.

Alisema baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakitoa kauli tata zinazoweza kuchochea taharuki, hivyo kamati ya uongozi ya baraza hilo itakutana na viongozi wa vyama vya siasa kuwakumbusha wajibu wao wa kisiasa kwa maslahi mapana ya nchi.

“Chanzo cha machafuko yoyote huanza na kauli, hivyo tumekuwa tukiwahimiza wanasiasa kuacha kauli zinazoleta uchochezi. Sasa hivi dunia ipo kwenye mtandao, hivyo kauli zinaweza kusababisha machafuko,” alisema Khatib.

Alisema kamati ya uongozi itafanya kazi ya kujenga siasa na kuondoa chuki za kisiasa nchini, ikiwemo baina ya vyama vya siasa na kati ya vyama hivyo na serikali iliyopo madarakani ili kujenga ukaribu zaidi wa kufanya kazi na jamii.

Khatib alisema kamati hiyo itaendeleza mazuri yaliyofanywa na kamati iliyopita, kwa kuhakikisha inaendeleza misingi ya demokrasia na kusimamia vyama vya siasa ili vifanye kazi kwa kuzingatia sheria za Msajili wa Vyama vya Siasa, Sheria ya Vyama vya Siasa na sheria nyingine za nchi.

Naye Mwenyekiti mpya wa Kamati ya Uchaguzi ya baraza hilo, Majalio Kyara alisema kamati hiyo ni chombo muhimu katika Baraza la Vyama vya Siasa na ina nafasi kubwa katika utengamano, ujenzi wa taifa na maendeleo ya demokrasia nchini.

“Nikiwa mwenyekiti wa kamati hii, hatua kubwa ambayo tutakwenda kuendelea nayo ni pamoja na masuala ya maridhiano ya kitaifa na kujenga umoja wa taifa letu la Tanzania,” alisema Kyara.

Kwa upande wake, Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania, Mohamed Ali Ahmed aliwataka viongozi wa kamati hizo kuwa mfano wa uwajibikaji na kutoa mwelekeo sahihi utakaosaidia kuimarisha umoja, mshikamano na amani nchini.

Aliwataka viongozi hao kutumia kauli za kiungwana na kiustaarabu zinazojenga na kuongeza kuwa kauli za chuki na uchochezi ni miongoni mwa mambo yanayochangia machafuko katika taifa lolote duniani.

Post a Comment

Previous Post Next Post