" BARRICK NORTH MARA, JUMUIYA YA WATUMIA MAJI WAFANIKISHA UPANDAJI MITI 47,200 KUHIFADHI MTO TIGHITE

BARRICK NORTH MARA, JUMUIYA YA WATUMIA MAJI WAFANIKISHA UPANDAJI MITI 47,200 KUHIFADHI MTO TIGHITE

 


Sehemu ya viongozi na wafanyakazi wa Barrick North Mara (kulia), viongozi wa Jumuiya ya Watumia Maji Mto Tighite Chini na Kijiji cha Matongo wakikagua maendeleo ya mradi huo Siku ya Mazingira Duniani 2026. (Picha za Maktaba)
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watumia Maji Mto Tighite Chini, Mwita Seri, akiwa kwenye kitalu cha miche ya asili inayooteshwa kwa ajili ya kupandwa kandokando ya Mto Tighite.
Ushirikiano wa Jumuiya ya Watumia Maji Mto Tighite (JWMT) na Kampuni ya Barrick kupitia Mgodi wake wa dhahabu wa North Mara umefanikisha upandaji wa miti ya asili 47,2000 kati ya 50,000 ambao utasaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na kulinda chanzo hicho cha maji kinachotegemewa katika shughuli mbalimbali za ustawi wa jamii na utunzaji wa mazingira.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watumiaji maji wa Mto Tighite, Bw. Mwita Seri amesema mradi huo unaotekelezwa kwa ufadhili wa Barrick North Mara unalenga kurejesha uoto wa asili na kuimarisha uhifadhi wa mto huo uliopo Nyamongo, Wilaya ya Tarime.

Amesema Tanzania kama zilivyo nchi nyingine duniani inakabiliwa na tishio la majanga yanayotokana na mabadiliko ya tabia nchi kutokana na uharibifu wa mazingira hususani kupitia kukata miti ovyo, shughuli za kilimo na kiuchumi.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Bw. Seri, mradi huo unalenga kurejesha uoto wa asili na kuimarisha uhifadhi wa mto huo uliopo Nyamongo, wilaya ya Tarime, mkoani Mara.

“Miti hiyo imepandwa katika eneo lenye ukubwa wa takriban ekari 40,” Seri amewaambia waandishi wa habari wilayani Tarime.

Amebainisha kuwa eneo lililopandwa miti hiyo ni sehemu ya ekari 100 za kingo za Mto Tighite zinazotakiwa kurejeshewa uoto wa asili kutokana na uharibifu wa mazingira.

Hivyo, upandaji wa miti 47,200 kwenye ekari 40 ni hatua ya awali katika safari ndefu ya kurejesha uoto wa asili wa Mto Tighite uliopo jirani na Mgodi wa North Mara.

Seri ameongeza mradi huo unatarajiwa kuchangia katika kulinda kingo za mto huo kwa kuzuia mmomonyoko wa udongo na kurejesha mazingira ya asili yaliyoharibiwa.

Mwenyekiti huyo wa Jumuia ya Watumia Maji, alitumia nafasi hiyo pia kuishukuru Barrick North Mara kwa kutoa shilingi milioni 36.7 kuwezesha uanzishaji na utekelezaji wa awali wa mradi huo.

“Barrick wamesaidia sana kufanikisha mradi huu, kwani fedha hizo ziligharamia uoteshaji wa miche ya miti ya asili, upandaji, ulinzi wa awali wa miti hiyo na uwekaji wa nguzo za chuma za uzio wa mradi huo,” amesema Seri.

Aidha, Seri ametoa wito kwa jamii zinazozunguka mto huo kuunga mkono mradi huo kwa kuhakikisha kuwa unafanikiwa bila kuhujumiwa kwa namna yoyote ile.

“Jamii inayozunguka Mto Tighite nayo ina wajibu wa kuonesha ushirikiano na juhudi za kulinda miti iliyopandwa ili iweze kukua na kutimiza lengo la kurejesha uoto wa asili wa mto wetu,” ameeleza.

Pia, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuwezesha mradi huo kifedha na kitaalamu ili kuhakikisha mafanikio yaliyoanza kuonekana yanaendelea kudumu na kuleta matokeo chanya ya muda mrefu kwa mazingira na jamii.

Mradi wa kurejesha uoto wa asili wa Mto Tighite unatajwa kuwa na umuhimu mkubwa wa kimazingira kutokana na nafasi ya chanzo hicho cha maji katika mfumo wa ikolojia ya eneo hilo.

Ulizinduliwa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani mwaka jana kwa lengo la kurejesha uoto wa asili wa mto huo unaotegemewa na maelfu ya watu kwa ajili ya maji ya matumizi ya nyumbani, kunywesha mifugo na shughuli za kilimo.

Hivi karibuni Mgodi wa North Mara uliungana na Jumuiya ya Watumia Maji Tighite Chini na wakazi wa kijiji cha Matongo kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani, kwa kutembelea na kukagua maendeleo ya mradi huo.

Wadau hao, wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kijiji cha Matongo, Charles Ryoba, walieleza kuridhishwa na ukuaji wa miti iliyopandwa na hatua zinazochukuliwa kurejesha uoto wa asili wa mto huo baada ya kuathiriwa na ukataji wa miti ovyo.

Ushirikiano wa Barrick North Mara na jumuiya hiyo unaweka msingi wa hatua zaidi za kuhusisha jamii, taasisi na wadau wengine katika kukamilisha upandaji wa miti ya asili kwenye ekari 100 za kingo za Mto Tighite.

Mto Tighite ni miongoni mwa vyanzo muhimu vinavyochangia maji katika Mto Mara ambao unamwaga maji yake katika Ziwa la kimataifa - Ziwa Victoria upande wa Tanzania.

Mbali na uwezeshaji wa kupanda miti maeneo yam to Tigheti , Barrick North Mara imekuwa mstari wa mbele kutekeleza sera ya kulinda mazingira kwa kuhakikisha inatumia uzalishaji kwa kutumia mifumo isiyoharibu mazingira sambamba na kushiriki kutoa elimu ya kulinda mazingira na vyanzo vya maji.

Vilevile wafanyakazi wake wamekuwa mstari wa mbele kushiriki katika miradi mbalimbali ya utunzaji wa mazingira.

Post a Comment

Previous Post Next Post