" CCM Yahimiza Amani, Yasisitiza Juhudi za Serikali Katika Ajira na Uchumi wa Vijana

CCM Yahimiza Amani, Yasisitiza Juhudi za Serikali Katika Ajira na Uchumi wa Vijana




CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesisitiza umuhimu kwa Watanzania kuendelea kulinda na kudumisha amani, umoja na mshikamano wa kitaifa, huku kikitaja tunu hiyo kuwa rasilimali isiyo na mbadala ambayo lazima ilindwe kwa wivu mkubwa.

Hayo yalisemwa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM anayeshughulikia Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenan Kihongosi, alipokuwa akizungumza kupitia kipindi cha Medani za Siasa kilichorushwa na kituo cha televisheni cha Star TV.

"Tutambue kwamba Taifa ni letu hatuna Taifa jingine, hapa Tanzania ndiyo nyumbani kwetu, ardhi yetu hii tuliyopewa na Mungu tuilinde kwa wivu mkubwa, kuna watu wanatamani kuja Tanzania, tusiharibu amani yetu kwa mikono yetu wenyewe," alisema Kihongosi.

Akizungumzia suala la ajira na uwezeshaji wa vijana, alieleza kuwa chama hicho kinaendelea kuisimamia Serikali ili kuhakikisha inajenga mazingira wezeshi ya kiuchumi kupitia mipango mbalimbali, ikiwemo utengaji wa asilimia 10 ya mapato ya halmashauri, mifuko ya uwezeshaji, na utoaji wa Sh. bilioni 200 kwa ajili ya vijana. Aliongeza kuwa kupitia ujenzi wa viwanda, kilimo, ufugaji, na uchimbaji wa madini, serikali inafungua milango ya fursa za kujiajiri na kuajiriwa kwa vijana.

Katika hatua nyingine, Kihongosi alitoa mwito kwa viongozi wa vyama vya siasa kufanya siasa za kistaarabu na zenye kutoa suluhisho badala ya kushambulia bila majawabu, huku akisisitiza kuwa haki na amani ni mambo yanayokwenda sambamba. Alihitimisha kwa kuwakumbusha vijana kuchangamkia fursa za kiuchumi na kutochagua kazi mradi iwe halali.

Post a Comment

Previous Post Next Post