Na Mwandishi Wetu
KAIMU Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC), Bi. Khadija Ngasongwa, amewataka wadau wa sekta ya umma na binafsi kuongeza ushirikiano katika mapambano dhidi ya bidhaa bandia, akisema biashara hiyo inahatarisha uwekezaji, ushindani wa haki na usalama wa watumiaji.
Ngasongwa ameyasema hayo leo Septemba 2, 2026 Jijini Dar es Salaam wakati akimwakilisha Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga, katika Kongamano la Ulinzi dhidi ya Bidhaa Bandia na Uwekezaji lililoandaliwa na Kampuni ya NANOSILIKAN kwa kushirikiana na FCC, TISEZA, TCCIA na TPSF, katika Hoteli ya Johari Rotana.
Amesema bidhaa bandia haziathiri ushindani wa kibiashara pekee, bali pia zinawaumiza wazalishaji wanaofuata sheria ambao hulipa gharama za ubunifu, upimaji, viwango, usajili, ajira na kodi, wakati wazalishaji wa bidhaa bandia huepuka gharama hizo na hivyo kushindana kwa njia isiyo ya haki.
“Katika ushindani wa kawaida, mzalishaji bora au mwenye ufanisi zaidi ndiye anayeshinda. Lakini kwenye bidhaa bandia, anayeshinda ni yule anayekwepa gharama zinazofanya bidhaa iwe halali,” amesema
Ngasongwa amesema athari kubwa zaidi ya bidhaa bandia humwangukia mlaji, akitolea mfano mbegu bandia ambazo mkulima anaweza kugundua tatizo baada ya msimu kupita, dawa ambazo hazitibu ugonjwa uliokusudiwa na vipuri bandia vya magari ambavyo vinaweza kuhatarisha usalama wa watumiaji. Alisema kwa kuwa madhara hayo yanaweza kujitokeza kabla ya hatua za kisheria kuchukuliwa, ni muhimu kuweka mifumo ya kuzuia bidhaa bandia kufika kwa mlaji.
Kwa mujibu wa Ngasongwa, utekelezaji wa sheria pekee hauwezi kumaliza tatizo hilo kwa kuwa maafisa wa ukaguzi hawawezi kuwepo katika kila duka na kila muamala nchini, hivyo ni muhimu kuwawezesha walaji kushiriki katika kuthibitisha uhalali wa bidhaa kabla ya kufanya manunuzi. Alisema njia hiyo inaweza kusaidia kuzuia madhara kabla hayajatokea, huku akisisitiza kuwa jukumu la Serikali la kusimamia sheria na kulinda walaji linaendelea.
Aidha, aliwataka wafanyabiashara na wazalishaji kutoa taarifa kwa FCC wanapobaini bidhaa zao zikighushiwa, kusajili na kutunza kumbukumbu za alama za biashara zao pamoja na kushirikiana katika kutoa taarifa kuhusu wahusika wa biashara ya bidhaa bandia.
Kongamano hilo limewakutanisha wawakilishi wa Serikali, taasisi za udhibiti, sekta binafsi, wafanyabiashara, taasisi zinazohusika na haki miliki pamoja na wadau wa maendeleo, kwa lengo la kujadili namna bora ya kulinda uwekezaji, wafanyabiashara na walaji dhidi ya athari za bidhaa bandia nchini.
Post a Comment