Na Alex Sonna, Dodoma
WAKALA wa Vipimo Tanzania (WMA) umeanza kuandaa kizazi cha mabalozi wa matumizi sahihi ya vipimo kupitia uanzishwaji wa Klabu za Vipimo katika shule za msingi, hatua inayolenga kuwajengea watoto uelewa wa mapema kuhusu haki za mlaji, uadilifu katika biashara na umuhimu wa vipimo sahihi katika kujenga uchumi shindani unaolengwa na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Hayo yameelezwa Septemba 18,2026 wakati wa mahafari ya wanafunzi wa darasa la saba Shule ya Msingi Mtemi Mazengo jijini Dodoma ambapo wanafunzi wa klabu ya vipimo walikuwa wakitoa elimu ya vipimo kwa wazazi na watu wengine mbalimbali waliohudhuria akiwemo Mgeni Rasmi.
Meneja wa WMA Mkoa wa Dodoma, Said Ibrahim, amesema mpango huo umetokana na maelekezo ya Mtendaji Mkuu wa WMA, Alban Kihulla, ya kuifikisha elimu ya vipimo kwa wananchi kuanzia ngazi ya shule, akieleza kuwa Shule ya Msingi Mtemi Mazengo ni miongoni mwa shule zilizoanzisha Klabu ya Vipimo ambayo imekuwa ikiwajengea wanafunzi uwezo wa kutambua na kuelewa matumizi sahihi ya vipimo katika maisha ya kila siku.
Amesema elimu hiyo tayari imeanza kuwa na matokeo katika jamii kwa kuwa wanafunzi hao wanapokwenda dukani kununua bidhaa kama sukari na unga, wanaweza kufuatilia kama kiasi walichopewa kinaendana na fedha walizolipa, ikiwemo kuangalia kama mizani inayotumika imehakikiwa na WMA, hivyo kuwafanya kuwa mabalozi wa elimu hiyo kwa wazazi, ndugu na wananchi wengine.
"Mwamko wa wanafunzi hao umeongezeka kiasi cha kuanza kutumia matukio mbalimbali ya kijamii kutoa elimu ya vipimo, akitoa mfano wa ushiriki wao katika maonesho ya Nane Nane yaliyofanyika mwezi Agosti, ambapo waliweza kueleza masuala ya vipimo kwa wananchi na viongozi mbalimbali, huku kwa sasa wakipanga kupanua uelewa wao kwa kutembelea vituo vya mafuta kujifunza namna vipimo vya mafuta vinavyofanya kazi."amesema Bw.Ibrahim
Akizungumzia mchango wa mpango huo katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Ibrahim amesema watoto wanaopatiwa elimu hiyo leo ndio watakaokuwa sehemu ya uongozi na shughuli za kiuchumi katika miaka ijayo, hivyo kuwajengea uelewa wa vipimo ni kuandaa jamii inayotambua thamani ya uadilifu, usawa na ushindani katika biashara.
Amesisitiza kuwa uchumi imara na shindani hauwezi kujengwa bila vipimo vinavyoaminika, kwa kuwa kila mwananchi anapaswa kupata thamani halisi ya bidhaa au huduma inayolingana na fedha anayolipa.
Kwa upande wake, Mlezi wa Klabu ya WMA katika Shule ya Msingi Mtemi Mazengo, Mwalimu Fadhili Mweruhanga, amesema klabu hiyo imekuwa nyenzo muhimu ya kuwafundisha wanafunzi kwa vitendo kuhusu vipimo, huku WMA ikiwezesha walimu na wanafunzi kupata vifaa vya kufundishia, jambo linalosaidia kujenga uelewa unaoweza kuhamishwa kutoka shuleni kwenda kwenye familia na jamii.
Amesema umuhimu wa klabu hiyo unaonekana katika mabadiliko ya tabia na uelewa wa wanafunzi, kwani sasa wanaweza kutumia maarifa wanayopata shuleni katika mazingira halisi, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha bidhaa wanazonunua zinatolewa kwa kipimo sahihi na mizani inayotumika ina alama ya WMA inayoonesha kuwa imehakikiwa.
Naye Mwanafunzi wa Klabu ya Vipimo katika Shule ya Msingi Mtemi Mazengo, Gloria Elisha Enock, amesema WMA imewajengea uwezo wa kuelewa maana na umuhimu wa vipimo pamoja na jukumu la Wakala la kumlinda mlaji.
Kwa upande wake, mwanafunzi mwenzake, Venosa Michael Simba, amesema elimu hiyo imemsaidia kubadilika kutoka kuwa mtoto anayekwenda dukani bila kuzingatia usahihi wa vipimo hadi kuwa mfuatiliaji na mtoa elimu kwa jamii.
Kwa ujumla, Klabu za Vipimo za WMA zimeanza kuwa darasa la vitendo la kuwaandaa watoto kuwa mabalozi wa ulinzi wa mlaji, huku elimu hiyo ikitoka shuleni na kuingia moja kwa moja katika familia na jamii.
Mpango huo unaongeza uelewa wa wananchi kuhusu matumizi ya vipimo sahihi, unasaidia kujenga utamaduni wa kuhoji na kuthibitisha vipimo vinavyotumika katika biashara na, kwa muda mrefu, unaweka msingi wa kizazi kinachothamini uadilifu, usawa na uwazi katika shughuli za kiuchumi.

Post a Comment