" MSIWAPIGE WAFANYABIASHARA WADOGO BALI WASIMAMIENI KWA KUTUMIA MIPANGO MIZURI - RAIS SAMIA

MSIWAPIGE WAFANYABIASHARA WADOGO BALI WASIMAMIENI KWA KUTUMIA MIPANGO MIZURI - RAIS SAMIA




RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka viongozi wa Serikali za Mikoa na Halmashauri kusimamia wafanyabiashara wadogo wanaofanya biashara mitaani kwa kutumia mipango mizuri badala ya kuwanyang’anya bidhaa au kuwafanyia vitendo vya ukatili.




Rais Samia ametoa agizo hilo leo Jumatano, Septemba 2, 2026, Ikulu Ndogo ya Tunguu, Zanzibar, wakati akizungumza baada ya kuwaapisha viongozi wateule.




Amesema licha ya Serikali kujenga masoko makubwa, wafanyabiashara wadogo wameanza kurejea mitaani kwa kasi, hivyo viongozi wanapaswa kutafuta suluhisho litakalowezesha wafanyabiashara hao kufanya biashara katika maeneo rasmi.




“Twende tukawasimamie si kwa kuwapiga fimbo kwa kutumia mgambo, kwa kuwanyang’anya vitu vyao na kuwapiga mateke hapana, bali kwa mipango mizuri itakayowafanya warudi kwenye masoko,” amesema Rais Samia.




Aidha, amezitaka Halmashauri kujenga masoko zaidi kwa kutumia rasilimali wanazoweza kuzitafuta, akisisitiza kuwa Serikali za Mitaa pia zina wajibu wa kuboresha mazingira ya biashara kwa wananchi.




“Halmashauri jitahidini mjenge masoko mengine, si kila soko kwenye Halmashauri zenu litajengwa na Serikali, nyinyi pia ni Serikali,” amesema.




Katika hatua nyingine, Rais Samia amewataka viongozi hao kusimamia usafi katika maeneo yao, akisema mazingira safi ni muhimu katika kuzuia magonjwa ikiwemo kipindupindu.




“Nendeni mkasimamie usafi katika maeneo yenu, usafi ni kila kitu, kupitia usafi mtaondosha maradhi yote ikiwemo kipindupindu,” amesema.




Amesisitiza kuwa miji mikubwa haipaswi kuwa michafu na viongozi wanapaswa kuhakikisha usafi unakuwa sehemu ya utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.


Post a Comment

Previous Post Next Post