" NDEJEMBI AAGIZA DAMPO LA PUGU LIBORESHWE

NDEJEMBI AAGIZA DAMPO LA PUGU LIBORESHWE




Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam na Halmashauri zake kuboresha hali ya Dampo la Pugu na kupuliza dawa za kuua wadudu katika maeneo ya makazi yanayozunguka dampo hilo ili kuwalinda wananchi dhidi ya magonjwa, hasa katika kipindi hiki cha mvua.

Akifanya ziara katika dampo hilo, Makamu wa Rais ameonesha kutoridhishwa na kutofautiana kwa takwimu za kiasi cha taka zinazopelekwa kila siku, hivyo kuagiza mamlaka kukaa pamoja na kuweka takwimu sahihi zitakazosaidia kupanga mikakati madhubuti ya usimamizi wa taka jijini.

Aidha, Makamu wa Rais ametoa muda wa siku saba kwa mawaziri wanaohusika na TAMISEMI, Maliasili na Utalii, na Ardhi kufika wenyewe katika eneo hilo ili kutatua mgogoro wa muda mrefu wa mipaka ya kiutawala na mpaka wa Msitu wa Kazimzumbwi unaowaathiri wakazi wa Pugu na maeneo ya jirani.

Wakazi wa maeneo ya Mstafa, Viwege, na Kinyamwezi walipata fursa ya kueleza kero zao ikiwemo ukosefu wa maji kwa muda mrefu na athari za dampo hilo, ambapo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ameahidi kusimamia kikamilifu maelekezo yote yaliyotolewa ili kupata ufumbuzi wa kudumu.

Post a Comment

Previous Post Next Post