" TANZANIA NA KOREA KUSINI ZASUKUMA MBELE USHIRIKIANO WA KIUCHUMI

TANZANIA NA KOREA KUSINI ZASUKUMA MBELE USHIRIKIANO WA KIUCHUMI




Serikali ya Tanzania na Jamhuri ya Korea Kusini zimefikia makubaliano ya kuharakisha utekelezaji wa ahadi ya dola za Marekani bilioni 2.5 zinazolenga kufadhili miradi mikubwa ya kimkakati nchini.

Katika mazungumzo yaliyofanyika pembezoni mwa Jukwaa la Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Korea na Afrika (KOAFEC) jijini Seoul, Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, aliongoza ujumbe wa Tanzania na kusisitiza umuhimu wa kuondoa vikwazo na ucheleweshaji uliokuwepo katika tafiti za upembuzi yakinifu na usanifu wa kihandisi chini ya Mfuko wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Kiuchumi wa Korea (EDCF).

Pande hizo mbili zimekubaliana kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi iliyoafikiwa wakati wa ziara ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan nchini humo, ikiongozwa na ujenzi wa Chuo Mahiri cha Tehama jijini Dodoma, sambamba na miradi mingine kama vile Kituo cha Kimataifa cha Mikutano na Maonesho Zanzibar, Hospitali ya Rufaa ya Binguni, uendelezaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, na ujenzi wa barabara ya Ifakara kwenda Mahenge inayohusiana na uchimbaji wa madini ya graphite, huku suala la ununuzi wa mabehewa ya SGR likifanyiwa mapitio ya pamoja ili liweze kutekelezwa kwa tija.

Wakati huo huo, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angelah Kairuki, alitumia jukwaa hilo kunadi fursa za uwekezaji wa kidijitali na kuwakaribisha wafanyabiashara wa Korea kuwekeza katika miundombinu ya mawasiliano, vituo vya kutunzia taarifa, upanuzi wa mtandao wa 5G, na huduma za Serikali Mtandao ili kuboresha utoaji wa huduma za jamii. Alibainisha kuwa ushirikiano huo unalenga pia kuimarisha teknolojia za kilimo, afya, na fedha, pamoja na kupata mitaji ya kuwezesha Shirika la Mawasiliano la Taifa (TTCL), kutumia nguvu kazi ya vijana wengi waliopo nchini ili kuzalisha ajira na kukuza uchumi kupitia uchumi wa kidijitali.

Majadiliano hayo yalihitimishwa kwa msisitizo wa kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa katika nyanja ya Akili Unde (AI) na miundombinu ya kisasa, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa malengo ya jukwaa la KOAFEC lililoandaliwa kwa ushirikiano na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Benki ya Exim ya Korea.

Post a Comment

Previous Post Next Post